Tuesday, December 7, 2010

WASANII BONGO WANAJIMALIZA WENYEWE


Mwanamuziki mkongwe nchini ambaye ni memba wa Bendi ya Kilimanjaro ‘Wananjenje’ John Kitime amesema kwamba, wasanii nchini wanajimaliza wenyewe kwa kukubali mikataba isiyo na maslahi kwao, kujichosha kwa maonyesho mengi yasiyo na mpangilio,kuishi maisha ya anasa kuliko uwezo wao,kunakiri hovyo kazi za nje na kutokuwa na umoja pia msimamo wa pamoja katika masuala yanayowahusu.
Kitime aliyasema hayo wakati akiwasilisha mada kwenye Jukwaa la Sanaa iliyohusu mwenendo wa muziki wa dansi nchini ambapo alisema kwamba, bendi nyingi zimekuwa na maonyesho mfululizo bila kujali kupumzika hali ambayo inawafanya wasanii wachoke, wakose ubunifu na kuwa wa kulala mchana kutwa hivyo kuporomoka kwa muziki wa dansi.

Kuhusu maisha duni na kudhulumiwa kwa haki zao,Kitime alisema kwamba, kunasababishwa na wasanii kuingia mikataba mibovu, kutokuwa na umoja katika kushinikiza haki zao, kukubali viwango vya chini vya malipo katika maonyesho, kutumia vibaya kile wanachokipata kwa anasa na kutotaka kujifunza juu ya haki zao mbalimbali kutokana na kulewa umaarufu na kukimbilia mafanikio ya haraka haraka.
“Msanii anapouza master yake unategemea nini? Ni sawa na mtu aliyeuza nyumba kwani anakuwa hana haki yoyote na aliyeiuza atakuwa na mamlaka ya kufanya chochote ikiwa ni pamoja na kuipangisha.Sasa aliyeuza nyumba atakuwa kichaa akienda kuhoji kupangishwa kwa nyumba ambayo amekwishaiuza na kupoteza haki ya umiliki.

Nashangaa sana,soda zina bei yake,bia zinapangiwa bajeti kwenye sherehe mbalimabli lakini linapokuja suala  la bajeti ya msanii,bei haipo inaanza kupangwa kwa kupigiana simu tu halafu kiwango kinakuja kuangukia laki moja.Ni aibu malipo ya wasanii kutokufahamika viwango wakati maji,soda na bia bei zake zinafahamika na wote tunalipa bila kujadili.Ni lazima wasanii watoke huko,wawe na viwango vya gharama vinavyokubalika kote” alisisitiza Kitime.

Aliongeza kwamba,baadhi ya wasanii wameingia mikataba ya kazi zao kutumiwa bure na vituo vya redio na TV huku wengine wakiingia mikataba ya ajabu na wasambazaji wa kazi zao hali ambayo inawanyima fursa ya kufaidi kazi zao na hivyo kuwaacha wafanyabiashara wakiwaburuza wasanii watakavyo.

Alizitaja changamoto mbalimbali za wasanii ambazo ni pamoja na kutokuwa uelewa wa haki zao, kulewa umaarufu,kutotaka kupanua weledi katika tasnia ya sanaa,kutumia muda mwingi katika kuponda raha kwa kile kidogo wanachokipata na changamoto nyingine nyingi.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU