Tuesday, February 22, 2011

SERIKALI BADO INASHUGHULIKIA MASUALA YA RAMBIRAMBI NA FIDIA



KAIMU MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Meck Sadick Serikali bado inashughulikia suala la rambirambi na fidia kwa walioathirika kutokana na mlipuko wa mabomu katika ghala la jeshi huko Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam.

Ametoa taarifa hiyo leo mchana (Jumatatu, Februari 21, 2011) wakati akitoa taarifa kwa wake 26 wa viongozi mbalimbali wa kitaifa walioambatana na Mke wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda kwenda kutoa msaada wa vitu mbalimbali kwa watu waliopata maafa kutokana na mlipuko wa mabomu hayo.

“Bado tunashughulikia suala la mkono wa pole kwa wafiwa, pia tunaangalia fidia kwa waliopata ulemavu wa kudumu... ni suala ambalo linaweza kuchukua muda kidogo lakini tumekamilisha mambo ya mazishi kwa kuwafikisha katika maeneo waliyotaka wenyewe wakazikwe,“ alisema.

Alisema Serikali iligharimia kusafirishwa miili ya watu wanne kwenda wilayani Rorya (Mara);  na miiili mengine mmoja mmoja kwenda Kyela (Mbeya); Kagera; Newala (Mtwara); Lushoto (Tanga) na Manerumango (Pwani).

Alisema hadi sasa kuna miili minne katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambayo bado haijatambuliwa, miwili kati ya hiyo ina majina na mwingine unafanyiwa uchunguzi wa kitabibu kwa sababu uliharibiwa vibaya na mlipuko na hautambuliwi ni wa jinsi ipi.

Akizungumzia kuhusu zoezi zima hadi sasa, Kaimu Mkuu huyo wa Mkoa alisema kwamba wanakabiliwa na changamoto ya kupata picha kamili ya ukubwa wa maafa kutokana na jinsi milipuko ilivyotokea na wamewaomba wenyeviti wa mitaa wawasadie kuratibu zoezi hilo.

“Tunakabiliwa na changamoto ya kubaini idadi kamili ni nyumba ngapi zimebomoka kabisa au kidogo na zinahitaji msaada wa aina gani, kuna ambazo zimebomoka kabisa, nyingine zimeezuliwa mapaa, ziko zilizoharibiwa ukuta mzima au sehemu tu, ziko zenye nyufa tu na nyingine ni fensi tu.“

Alisema kwa nyumba ambazo zimebomoka kabisa, wanawasiliana na Chama cha Msalaba Mwekundu na Idara ya Maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu na kuwajengea mahema ili waweze kuendelea kuwepo katika eneo walilokuwa wakiishi.

“Kama nyumba ilikuwa na vyumba vitatu, tunawajengea mahema matatu ili kuwastahi wakubwa na watoto wakiwa katika mahema tofauti wakati taratibu nyingine zikiendelea. Kama nyumba ilikuwa na wapangaji wanne kila mmoja na chumba chake nao pia tunawajengea mahema manne ili wawe na maisha yaleyale,“ alisema.

Misaada iliyotolewa ni kilo 200 za mchele, kilo 100 za sukari, kilo 500 za unga wa mahindi, mafuta ya kujipaka katoni moja, sabuni za kufulia katoni moja, dawa za meno katoni moja, doti za khanga 55 ambayo ina thamani ya sh. milioni 1.5/-. Pia walitoa mabegi matatu ya nguo za wakubwa na watoto ambazo thamani yake haikuweza kupatikana mara moja.

Baadhi ya wake wa viongozi walioambatana Mama Pinda ni Mke mkubwa wa Makamu wa Rais, Bi. Zakia Bilal, Mke mdogo wa Makamu wa Rais, Bi. Asha Bilal, Mama Regina Lowassa, Mama Esther Sumaye, Mama Hasina Kawawa, na wake wa Mawaziri, Naibu Mawaziri na Makatibu wakuu.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU