Tuesday, February 22, 2011

KANUMBA: TUSILAUMIWE KUPOROMOKA KWA MAADILI

Muigizaji wa filamu nchini,Steven Charles Kanumba (Katikati) akiwasilisha mada kwenye Jukwaa la Sanaa kuhusu Harakati za kuivusha tasnia ya filamu katika ngazi za kimataifa.Kulia kwake ni Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego na Mratibu wa jukwaa hilo,Ruyembe C.Mulimba.
Mratibu wa Jukwa la Sanaa,Bw.Ruyembe akisisitiza jambo juu ya harakati za kuivusha tasnia ya filamu kwenye ngazi ya kimataifa.Katikati ni muigizaji Kanumba na Katibu Mtendfaji wa BASATA,Materego.
                 Mdau wa Sanaa Elimathew Kika akitoa mchango wake kwenye Jukwaa la Sanaa.
 Mjumbe wa Shirikisho la Sanaa za Maonyesho,Nkwama Bhalanga alitaka ufafanuzi ni kwa nini majina ya filamu yanakuwa ya kiingereza wakati maudhui ni kwa lugha ya Kiswahili.
             Sehemu ya wadau 207 waliohudhuria kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii wakifuatilia mada kwa makini.

                                              
Muigizaji maarufu wa filamu nchini Steven Charles Kanumba ameibuka na kusema kwamba, wasanii si chanzo cha kuporomoka kwa maadili katika jamii bali tatizo hilo linasababishwa kwa kiasi kikubwa na utandawazi unaombatana na mabadiliko ya teknolojia duniani.

Akiwasilisha mada kuhusu Harakati za kuivusha tasnia ya filamu katika ngazi za kimataifa kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu kwenye Ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Kanumba alipuuza malalamiko kwamba, wasanii wa filamu wamekuwa chanzo cha kuipotosha jamii kupitia yale wanayoyaigiza na kusema kwamba,malezi na utandawazi ni tatizo kubwa kwa sasa katika taifa na wazazi hawana budi kudhibiti watoto wao ili kuwaepusha na wimbi hili.

“Maadili hayako katika filamu tu,tunapozungumzia maadili ni katika nyanja nyingi.Leo mtoto mwenye miaka tisa anamiliki simu tena yenye internet,humo anaangalia facebook na picha za ajabu halafu mtoto huyu akiharibika watu wanasema ni filamu,hii si kweli” alisisitiza Kanumba ambaye amecheza zaidi ya filamu 40 hadi sasa.
Aliongeza kwamba,kwa kawaida wanapoandaa filamu wamekuwa wakiandika umri wa watazamaji wake lakini wazazi wengi wamekuwa wakipuuza na kuwaacha watoto kuangalia filamu ambazo hawapaswi kuangalia.Alitaja filamu kama ya This Is It ambayo anasema kuna watoto hawaruhusiwi kuiangalia lakini wazazi na walezi wengi wanapuuza hilo.

“Filamu zetu tunazotengeneza zinakuwa na ujumbe kwa jamii,zinabeba masuala yaliyomo ndani ya jamii.Suala la nani aangalie kilichomo tumekuwa tukiziwekea umri wa watazamaji.Naomba mniambie jamani hayo tunayoyaonyesha katika filamu yetu hayapo katika jamii?Na kwa nini sasa tulaumiwe kwa mambo ambayo yako ndani ya jamii zetu” alihoji Kanumba.

Akizungumzia suala la wao kuwa waongozaji,waandishi wa simulizi (script writers) na watafutaji mandhari (location) katika filamu moja,Kanumba alisema kwamba,ni suala la kawaida na limekuwa likifanyika katika nchi mbalimbali duniani na mara nyingi hufanywa ili kukwepa mlolongo mrefu na pia kubana matumizi.
Juu ya wizi katika kazi zao,Kanumba alisema kwamba,Chama cha hakimiliki (Cosota) kimekuwa kikijtahidi lakini tatizo limekuwa kwenye nguvukazi ya mamlaka hiyo lakini pia sheria ambazo zinaonekana hazikidhi matakwa.

Hata hivyo,akizungumzia hilo kwa niaba ya Cosota,Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego alisema kwamba,sheria mpya za hakimiliki ziko katika kiwango cha kupelekwa bungeni kwa ajili ya kupitishwa na uwezekano mkubwa ni kwenye bunge lijalo la mwezi wa nne.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU