MICHUANO YA KOMBE LA KAGAME 2011
Michuano ya kuwania Kombe la Kagame iliyofanyika nchini kuanzia Juni 25 hadi Julai 10 mwaka huu imekwenda vizuri huku timu za Tanzania, Yanga na Simba zikifanya vizuri kwa kufika hatua ya fainali. TFF tunazipongeza timu hizo kwa uwakilishi mzuri ziliotupa, hasa Yanga kwa kuibuka mabingwa.
Shukrani za pekee tunatoa kwa mashabiki waliojitokeza kushuhudia mechi za michuano hiyo zilizofanyika katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Mahudhurio ya washabiki katika mechi zote yaliingiza jumla ya sh. bilioni 1.073. Fedha hizo zimetuwezesha kulipia gharama zote za mashindano.
Pia tunatoa shukrani kwa wadau wengine waliowezesha mashindano hayo kufanikiwa wakiwemo wadhamini, hoteli, kampuni za usafiri, ulinzi, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, waandishi wa habari Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na klabu ya TCC Chang’ombe kwa kutoa viwanja vya mazoezi na Serikali kwa kutoa Uwanja wa Taifa.
Hoteli hizo ni Safina, Landmark, Lunch Time, Marriot, Paradise City, Valentino, Spice Inn, Blue Pearl, Akubu na Jangwani Plaza za Dar es Salaam. Oasis, Top Life na Kingston za Morogoro.,
Licha ya mafanikio hayo, tunawaomba radhi mashabiki kutokana na kukatika umeme kwenye Uwanja wa Taifa baada ya mechi ya fainali kati ya Yanga na Simba. Tukio hilo lilitokea wakati wa kukabidhi zawadi kwa timu mbalimbali zilizofanya vizuri katika mashindano hayo.
USAJILI WA WACHEZAJI
Kipindi cha uhamisho wa wachezaji kwa msimu wa mwaka 2011/2012 kinamalizika Julai 15 mwaka huu wakati mwisho wa usajili ni Julai 20 mwaka huu.
Kwa upande wa klabu za Ligi Kuu, usajili wao unaanzia kwa timu za pili (U20), hivyo kwanza zinatakiwa kukabidhi usajili wa timu hizo na baadaye za timu zao za kwanza (senior). Klabu zote za Ligi Kuu tayari zina passwords zao kwa ajili ya kufanya usajili wa wachezaji wa kigeni.
Dirisha dogo la usajili litafunguliwa tena Novemba 1 hadi 30 mwaka huu. Tunazikumbusha timu zote za Ligi Kuu kuwasilisha majina ya viwanja ambavyo zitatumia kwa ajili ya ligi hiyo ambayo itaanza Agosti 20 mwaka huu.
Klabu ambazo zimewasilisha maombi ya viwanja ambavyo zitatumia ni Mtibwa Sugar (Manungu), Azam (Chamazi), Ruvu Shooting Stars (Mlandizi), Coastal Union (Mkwakwani), Toto Africans (CCM Kirumba), Oljoro JKT (Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid Kaluta), Polisi Tanzania (Jamhuri, Dodoma) na Kagera Sugar (Kaitaba).
Klabu ambazo bado hazijawasilisha viwanja vyao ni Yanga, Simba, Moro United, Villa Squad, JKT Ruvu na African Lyon. Timu hizo zinatakiwa kutuma majina ya viwanja vyao haraka, kwani kabla ya kuruhusiwa kutumika ni lazima vithibitishwe na Kurugenzi ya Ufundi ya TFF.





0 maoni:
Post a Comment