Chama cha Mpira wa Miguu Sudan (SFA) kimefuta mechi ya kirafiki kati ya Taifa Stars na timu ya Taifa ya nchi hiyo ‘Nile Crododile’ iliyokuwa ichezwe Agosti 10 mwaka huu.
Uamuzi huo umetokana na wakala wa mechi hiyo Hadi Sharkawy kushindwa kupata kwa wakati tiketi ya kuisafirsha Taifa Stars kwenda Khartoum. Pia kutokana na mechi hiyo kufutwa, kambi ya Stars iliyokuwa hapa Dar es Salaam nayo imevunjwa leo.
LYON YAPEWA HADI AGOSTI 17 KULIPA WACHEZAJI
Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji iliyokutana Agosti 7 mwaka huu kupitia masuala mbalimbali imeiagiza klabu ya African Lyon iwe imewalipa wachezaji wake wawili kufikia Agosti 17 mwaka kwa kuvunja mikataba yao na klabu hiyo. Wachezaji ambao kila mmoja anadai sh. milioni 4.3 ni Godfrey Komba na Abdul Masenga.
Awali kamati hiyo katika kikao chake cha Januari 7 mwaka huu iliagiza klabu hiyo kutosajili mchezaji mpya msimu wa 2011/2012 hadi itakapokuwa imemaliza suala la wachezaji hao. Lyon imeomba kusajili wachezaji wapya wanane kati ya 23 inayotaka kuwatumia kwa msimu mpya.
Kwa kuzuiwa kusajili wachezaji wapya iwapo haitakuwa imemalizana na Komba na Masenga kufikia Agosti 17, Lyon itakuwa imebaki na wachezaji 15 hivyo kikanuni kutokuwa na sifa ya kushiriki Ligi Kuu ya Vodacom. Kanuni inaagiza timu inayoshiriki ligi hiyo kuwa na wachezaji wasiopungua 18 na kuzidi 30.
PINGAMIZI LA YANGA DHIDI YA SIMBA
Kamati haikusikiliza pingamizi la Yanga dhidi ya Simba kuhusu wachezaji iliyotoa kwa mkopo baada ya kubaini kuwa wachezaji ambao Simba imewatoa kwa mkopo ni wane tu; Haruna Shamte (Villa Squad), Aziz Gilla (Coastal Union), Ahmed Shiboli (Kagera Sugar) na Mohamed Kijuso (Villa Squad).
Wachezaji wengine waliotajwa na Simba kupelekwa kwa mkopo katika klabu mbalimbali ilibainika kuwa ni wa kikosi cha pili (U20) ambao hawahusiki na kanuni ya mkopo. Wachezaji wanaoweza kutolewa kwa mkopo ni wa kulipwa tu (wenye mikataba).
Kwa upande wa Athuman Idd na Juma Jabu ambao hawakuonekana kwenye orodha ya usajili ya Simba, kamati imesema ni wachezaji halali wa klabu hiyo kwa vile wana mikataba nayo. Idd ana mkataba wa miaka miwili wakati Jabu mkataba wake umebakiza mwaka mmoja kumalizika. Kamati imesisitiza kuwa kitu kikubwa kinachoangaliwa kwenye usajili wa wachezaji wa Ligi Kuu ni mikataba na si kusaini fomu za usajili.
MCHEZAJI AMANI PETER KYATA
Kyata aliombewa usajili katika klabu mbili za African Lyon na Yanga. Lyon walimuombea kwa timu ya wakubwa, wakati Yanga walimuorodhesha katika timu ya pili (U20).
Kamati ilibaini kuwa mchezaji huyo ni wa kituo cha Tanzania Soccer Academy (TSA) kinachomilikiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na hakuna mchakato wowote uliofanyika kumsajili, hivyo usajili wake haujakamilika Yanga wala Lyon.
SUALA LA MCHEZAJI OSCAR JOSHUA
Sekretarieti ya TFF imeelekezwa kupeleka suala la mchezaji huyo Polisi kwa ajili ya uchunguzi kwa vile kuna barua mbili zinazopingana kutoka timu yake ya Ruvu Shooting- ya kwanza ikiridhia achezee Yanga na ya pili ikipinga kuwa taratibu hazikufuatwa katika kujiunga na timu yake mpya.
Uamuzi huo wa kamati umelenga kubaini ipi ni barua halali kati ya mbili zilizowasilishwa TFF kuhusu usajili wake Yanga, na zote zikionesha kutoka katika timu yake ya Ruvu Shooting.
Pia kamati imeamua kuwa kwa vile TFF ilifanyia kazi barua ya kwanza ya kumruhusu kwenda Yanga, hivyo kumpatia leseni, mchezaji ataendelea kutumia leseni hiyo hadi taarifa ya uchunguzi wa Polisi kuhusiana na barua hizo mbili itakapotolewa.
HARUNA MOSHI v POULSEN
Kuhusu mchezaji Haruna Moshi ‘Boban’ kutoitikia mwito wa Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen kucheza mechi kati ya U23 na Shelisheli zilizofanyika Arusha, kamati kwa sasa imeliacha suala hilo kwa kocha huyo kwa vile kuna maagizo ametoa kwa mchezaji huyo.
Poulsen amemtaka Boban binfasi kwenda kumueleza sababu ya kutoitikia mwito wake wa kucheza mechi dhidi ya Shelisheli kabla hajafanya uamuzi mwingine kuhusu mchezaji huyo.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 maoni:
Post a Comment