Saturday, September 24, 2011

FAINALI ZA MCHEZO WA VISHALE ZAPAMBA MOTO TANGA

Fainali za Mashindano ya kitaifa ya mchezo wa Safari Darts yameanza kutimua vumbi mkoani Tanga kwa kushirikisha mikoa tisa ya Tanzania Bara ambapo yameelezewa kuwa na msisimko mkubwa kulinganisha na miaka iliyopita.

Mwenyekiti wa Taifa wa chama cha Darts Nchini,Bwana. Gisase Waigana alisema mashindano ya mwaka huu yamekuwa na mafanikio makubwa hasa kutokana na udhamini walioupata toka Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Safari Lager.

Alisema mchezo wa Darts umekuwa haupewi nafasi sana miongoni mwa jamii na kuiomba jamii kuwekea mkazo mkubwa kwenye mchezo huo ikiwa ni pamoja na kujifunza na hatimae kuweza kuleta tija na mafanikio makubwa kwenye Nyanja za kimataifa.

Alisema mashindano ya mwaka huu yametoa mwanga kwa serikali kutaka uwezekano wa kuweka mchezo huu kwenye mitaala ya masomo ili kuweza kuukuza vyema badala ya kuendelea kuweka nguvu kwenye mchezo mmoja huku wakisahau kuwa watanzania wanahitaji kuona mafanikio na kushangilia ushindi.

Mashindano ya Mwaka huu yameshirikisha mikoa tisa kati ya mikoa kumi na sita  ambapo hadi leo kwenye mchezo wa mmojammoja wana dada waliofanikiwa kuingia fainali ni Fabiola Namajojo toka Morogoro,Agness Kweka toka Kilimanjaro,Vick Kipendaroho toka Morogoro na Cecilia Robert toka Mwanza. Wakati wanaume ni Sanjay Karan Toka Dar Es Salaam dhidi ya Rumba Ismail toka Dar Es Salaam wakati mchezaji wa kwanza kutinga fainali ni Wambura Msila toka Morogoro.

Kwa upande wao baadhi ya wachezaji waliomba kuwepo na mashindano ya mara kwa mara ili kuweza kuwapa nafasi ya kujiandaa vyema na kuwaomba vijana kujitokeza kwa wingi kwenye kujifunza na kucheza ili kuweza kujiwekea nafasi ya ushindani zaidi kwa siku za Usoni.

Mashindano hayo yalifunguliwa na Mwenyekiti wa taifa wa Baraza la michezo la Taifa,Col Mstaafu Iddy Omary Kipingu ambapo katika salam zake aliwataka wachezaji wa Darts kuonyesha ushirikiano mkubwa na juhudi huku akisema serikali ipo tayari kushirikiana na wadau mbalimbali kwenye kuukuza na kuundeleza mchezo huo.

Alisema TBL kupitia bia yake ya Safari Lager imekuwa mfano wa kuigwa katika kuibua na kuendeleza michezo mbalimbali nchini toka katika ngazi za chini jambo ambalo ni la muhimu kuliko kitu chochote katika kuundeleza michezo nchini.

"Nawaomba wenzetu TBL kuendelea na moyo huu huu walionao , wao wanasema ni katika juhudi za kurejesha faida ndogo kwa watanzania katika kuendeleza michezo nchini lakini naomba na wengine nao waige mfano toka TBL" alisema Kipingu.

Kwa upande wake Meneja wa Bia ya Safari Lager, Bwana Oscer Shelukino alisema Safari Lager itaendelea kukuza na kuibua vipaji kwenye Nyanja mbalimbali za kimichezo ambapo tayari Safari Lager inadhamini Mashindano ya Pool, Nyama Choma,Tuzo za Shujaa wa Safari na Sasa ikidhamini mashindano haya ya Darts Taifa.

Mashindano haya yanatarajia kufungwa kesho jumapili na meya wa manspaa ya Tanga.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU