Monday, September 26, 2011

LESENI KWA KLABU ZA VPL

LESENI KWA KLABU ZA VPLKlabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zimekumbushwa kutekeleza kikamilifu makubaliano ya Azimio la Bagamoyo (Bagamoyo Declaration) katika semina iliyofanyika mwaka 2007 mjini Bagamoyo kati yao na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA). 

Kamati ya Mashindano ya TFF iliyokutana Septemba 24 mwaka huu imesisitiza utekezaji wa azimio hilo ambalo lilifanyiwa tathmini ya kwanza chini ya FIFA Februari mwaka huu katika semina nyingine iliyofanyika hoteli ya Whitesands jijini Dar es Salaam kwani ni moja ya masharti ya kupata leseni kwa klabu za Ligi Kuu.

Pia Kamati hiyo chini ya uenyekiti wa Makamu wa Pili wa Rais wa TFF, Ramadhan Nassib imependekeza utekelezaji wa azimio hilo uanzie kwa klabu za Ligi Daraja la Kwanza ili kuziweka katika mazingiza mazuri ya utendaji zinapoingia Ligi Kuu.

Masuala ambayo yanatakiwa kutekelezwa na klabu hizo kwa mujibu wa Azimio la Bagamoyo ni kuwa na Katiba inayozingatia Katiba mfano (standard statute) iliyotolewa na TFF, kuajiri Sekretarieti kwa kuzingatia sifa za kitaaluma, kuwasilisha hesabu za fedha zilizokaguliwa kila mwaka kuanzia msimu wa 2010/2011.

Klabu kutenganisha majukumu ya kamati ya utendaji na Sekretarieti, benchi za ufundi kuongozwa na watu wenye sifa kwa mujibu wa kanuni za TFF (makocha na daktari wa tiba ya michezo), kuwa na timu za vijana hatua kwa hatua (U14, U17 na U20) na ofisi za kudumu (physical address).

Vilevile kuwa na uwanja wa kudumu wa mazoezi (kwa kuumiliki au wa kukodi kwa muda mrefu), vifaa vya kutosha vya mazoezi (kits, equipment na gym) na vifaa vya tiba ya michezo. Kamati ya Mashindano imeweka msisitizo katika hilo kwa vile TFF iko mbioni kuhakikisha timu zote zinazocheza Ligi Kuu zinakuwa na leseni kwanza baada ya kutimiza masharti hayo. Kwa mantiki hiyo kupanda daraja kutokuwa sifa pekee ya kucheza Ligi Kuu.

Hatua hiyo pia imelenga kuziweka tayari klabu za Tanzania Bara ambazo timu zake zitashiriki michuano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).  CAF imesema kuanzia msimu wa 2012/2013 ni klabu zenye leseni yake tu ndizo zitashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho. 

VIINGILIO YANGA vs COASTAL UNION.
Pambano namba 51 la Ligi Kuu ya Vodacom kati ya mabingwa watetezi Yanga na Coastal Union litachezwa Septemba 28 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.  

Viingilio vilivyopangwa katika mechi hiyo ni sh. 3,000 kwa viti vya bluu na kijani, sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa. VIP C ni sh. 7,000, VIP B ni sh. 10,000 na VIP A itakuwa sh. 15,000.

SHOOTING YAPIGWA FAINI SH. 

500,000Kamati ya Mashindano ya TFF imeipiga faini ya sh. 500,000 timu ya Ruvu Shooting ya Mkoa wa Pwani baada ya kupata kadi sita kwenye mechi namba 40 ya Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya Coastal Union iliyochezwa Septemba 17 mwaka huu Uwanja wa Mlandizi. Kwa mujibu wa Kanuni namba 25 (1)(d) ya Ligi Kuu ya Vodacom, timu ambayo wachezaji wake wataoneshwa zaidi ya kadi tano katika mechi moja itatozwa faini ya sh. 500,000.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU