Na Mwandishi Wetu
Warembo wanaoshiriki mashindano mbalimbali ya urembo nchini wameaswa kutovutwa na zawadi katika kujiingiza kwenye fani hiyo na badala yake wavutwe na wito katika kuitumikia jamii katika nyanja mbalimbali.
Wito huo umetolewa wiki hii na wadau wa Jukwaa la Sanaa linalofanyika kwenye Ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ambapo walisema kwamba,kuvutwa na zawadi katika kushiriki mashindano hayo ni chanzo cha warembo hao kuingia kwenye vishawishi kutokana na wengi wao kutomudu zawadi hizo.
“Warembo wengi wamekuwa wakijitokeza kushiriki mashindano ya urembo,ukiwauliza ni nini kimewavuta watakwambia ni zawadi.Tatizo linaanza pale wanapopewa zawadi kama magari ambayo wanashindwa kuyamudu hivyo kujiingiza kwenye vishawishi” alisema mdau mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Kelvin.
Aliongeza kwamba,Duniani kote warembo wanaoshiriki mashindano ya urembo huvutwa na matatizo yaliyo ndani ya jamii kama umaskini, mauaji ya vikongwe, imani potofu zilizo katika jamii, watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na mengineyo.
Kwa mujibu wa mdau huyo,hata mashindano ya urembo yanayofanyika hapa nchini kila mwaka lazima yawe na kaulimbiu yake badala ya ilivyo sasa ambapo yamekuwa hayabebi ujumbe au dhana yoyote na hivyo kutokueleweka mwelekeo.
Awali akiwasilisha mada kuhusu Historia ya Shindano la Miss Utalii na Changamoto zake Rais wa shindano hilo hapa nchini,Gideon Chipungahelo alisema kwamba, shindano lake limekuwa likisimamia nguzo kuu tano ambazo ni asili, utamaduni, utalii,mitindo na urembo.
“Shindano la Miss Utalii linasimamia utanzania na asili yetu, unapata five in one (vitu vitano ndani ya kimoja) ambavyo ni asili, utamaduni,utalii,mitindo na urembo” alisisitiza Chipungahelo.
Alizitaja changamoto zinazolikabili shindano hilo kuwa ni pamoja na kukosekana kwa wadhamini, kuwepo kwa watu wanaoilipiga vita shindano hilo kwa sababu ambazo hakuzitaja, warembo wengi wanaojitokeza kuvutwa na zawadi badala ya kuitumkia jamii na changamoto nyingine.
Jukwaa la Sanaa ni programu inayoandaliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari za Sanaa na Utamaduni (CAJAtz) na hufanyika kila Jumatatu kwenye Ukumbi wa BASATA.
0 maoni:
Post a Comment