Friday, November 11, 2011

STARS YAONA MWEZI YASHINDA 2-1

Kocha wa Taifa Stars, Jan Poulsen amepata ushindi wake wa kwanza ugenini tangu alipochukua timu hiyo
kutoka kwa Mbrazil Marcio Maximo, Agosti mwaka jana baada ya leo kuifunga Chad mabao 2-1 katika
mechi ya kwanza ya mchujo ya makundi ya fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwaka 2014 nchini
Brazil.
 
Ikicheza kwa mara ya kwanza nchini Chad, Stars ndiyo iliyokuwa ya kwanza kufunga dakika ya kumi
katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Idriss Mahamat Ouya hapa N'Djamena kupitia kwa winga
Mrisho Ngasa.
 
Hata hivyo, mashabiki wa Chad walisubiri kwa dakika tano tu kabla ya kusherehekea bao baada ya kiungo
Mahamat Labo kuisawazishia dakika ya 15. Labo anachezea klabu ya Laval ya Ufaransa alitumia vizuri
makosa ya mabeki wa Tanzania waliochelewa kucheza mpira wa krosi.
 
Dakika kumi kabla ya mwamuzi Bunmi Ogunkolade kutoka Nigeria hajapuliza filimbi ya kuhitimisha
pambano hilo lililohudhuriwa na takribani mashabiki 10,000, Nurdin Bakari aliyeingia badala ya Abdi
Kassim aliifungia Stars bao la pili.
 
Mpira ulianzia kwa mshambuliaji wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Thomas
Ulimwengu ambaye akiwa wingi ya kulia alifanikiwa kumtoka beki wa kushoto wa Chad kabla ya
kutumbukiza krosi iliyomkuta mfungaji.
 
Stars na Chad zinakutana tena Jumanne kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi ya
marudiano ambayo matokeo yake ndiyo yataamua timu ipi kati ya hizo itakayoingia hatua ya makundi,
kwenye kundi ambalo lina timu za Ivory Coast, Morocco na Gambia.
 
Stars: Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Idrisa Rajab, Aggrey Morris, Juma Nyoso, Shabani Nditi, Nizar
Khalfan/Thomas Ulimwengu, Henry Joseph, Mbwana Samata/Mohamed Rajab, Abdi Kassim/Nurdin Bakari
na Mrisho Ngassa.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU