Thursday, November 24, 2011

TENGA ACHAGULIWA TENA CECAFA


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amechaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
 
Tenga amechaguliwa leo (Novemba 24 mwaka huu) bila kupingwa baada ya mpinzani wake Fadoul Hussein wa Djibouti kutotokea kwenye uchaguzi.
 
Kutokana na hali hiyo, mjumbe kutoka Uganda alitoa hoja ya Tenga kupitishwa bila kupingwa, hoja ambayo iliungwa mkono na Kenya, Tanzania, Uganda, Sudan, Zanzibar, Ethiopia, Burundi na Eritrea.
 
Jumla ya nchi wanachama zilizopiga kura katika uchaguzi uliofanyika hoteli ya New Africa ni kumi na moja, na kila moja ilikuwa na kura moja tu.
 
Kwa upande wa nafasi nne za wajumbe wa Kamati ya Utendaji kulikuwa na wagombea wanane. Waliopita katika raundi ya kwanza na kura zao kwenye mabano ni Abdiqani Saeed Arab wa Somalia (8), Tariq Atta Salih wa Sudan (8) na Raoul Gisanura wa Rwanda (8).
 
Wengine katika raundi ya kwanza na kura walizopata kwenye mabano ni  Sahilu Wolde wa Ethiopia (4), Justus Mugisha wa Uganda (4), Tesfaye Gebreyesus wa Eritrea (4), Hafidh Ali Tahir wa Zanzibar (2) na
Abubakar Nkejimana wa Burundi (3).
 
Mjumbe aliyefanikiwa kushinda katika raundi ya pili na kuingia kwenye Kamati ya Utendaji ni Wolde wa Ethiopia aliyepata kura tano dhidi ya nne za Mugisha na mbili za Gebreyesus.
 
Mwenyekiti anakaa madarakani kwa miaka minne wakati wajumbe wa Kamati ya Utendaji wanachaguliwa kila baada ya miaka miwili.
 
ZIMBABWE YAZIBA NAFASI YA NAMIBIA
Timu ya Taifa ya Zimbabwe (Might Warriors) imeteuliwa na CECAFA kushiriki michuano ya Kombe la Chalenji inayoanza Novemba 25 mwaka huu jijini Dar es Salaam kuziba nafasi ya Namibia iliyojitoa.
 
Zimbabwe itawasili Novemba 26 mwaka huu jijini Dar es Salaam na itakuwa kundi A pamoja na timu za Tanzania Bara, Rwanda na Djibouti.
 
KIKOSI CHA KILIMANJARO STARS
Kocha Mkuu wa timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), Charles Boniface Mkwasa ametaja kikosi cha mwisho cha wachezaji 20 kwa ajili ya michuano hiyo inayoanza kesho.
 
Wachezaji waliobaki kati ya 28 waliokuwa wameitwa awali ni Juma Kaseja (Simba), Shabani Kado (Yanga), Shomari Kapombe (Simba), Godfrey Taita (Yanga), Juma Jabu (Simba), Ibrahim Mwaipopo (Azam) na Juma Nyoso (Simba), Said Murad (Azam), Erasto Nyoni (Azam) na Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Nurdin Bakari (Yanga), Haruna Moshi (Simba) na Mwinyi Kazimoto (Simba).
 
Wengine ni Said Maulid (Angola), Musa Mgosi (DC Motema Pembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC), Mrisho Ngassa (Azam), Ramadhan Chombo (Azam), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC) na Rashid Yusuf (Coastal Union).
 
Kilimanjaro Stars itacheza mechi yake ya kwanza Novembe 26 mwaka huu dhidi ya Rwanda.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU