Mji wa Morogoro ndiyo utakaokuwa mwenyeji wa kituo cha Fainali ya Tisa Bora ya Ligi Daraja la Kwanza kuwania nafasi tatu za kucheza Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2012/2013 itakayoanza Machi 31 mwaka huu.
Chama cha Mpira wa Miguu wa Morogoro (MRFA) ni baadhi ya vyama vya mikoa vilivyokuwa vimeomba kuwa mwenyeji wa fainali hizo huku chenyewe kikitimiza sehemu kubwa ya vigezo vilivyowekwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Vyama vingine vya mpira wa miguu vilivyokuwa vimeomba kuwa mwenyeji wa fainali hizo zinazoshirikisha timu tisa vilikuwa vya mikoa ya Mbeya, Mwanza, Ruvuma na Tabora.
Fainali hizo zitafanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini humo chini ya usimamizi wa TFF.
Timu zilizofuzu kucheza hatua ya fainali kutoka kundi A ni Polisi ya Dar es Salaam, Mgambo Shooting ya Tanga na Transit Camp ya Dar es Salaam. Kundi B ni Mbeya City Council, Mlale JKT ya Ruvuma na Tanzania Prisons ya Mbeya wakati kundi C ni Polisi ya Tabora, Polisi ya Morogoro na Rhino Rangers ya Tabora.
Wakati huo huo, mechi kati ya Temeke United na Small Kids kupata timu moja ambayo itakabaki Ligi Daraja la Kwanza na nyingine itakayoshuka itachezwa Machi 31 mwaka huu Uwanja wa Jamhuri, mjini Dodoma.
Kamati ya Ligi ya TFF iliyokutana Machi 12 mwaka huu iliamua timu hizo ambazo zilishika nafasi ya mwisho katika makundi yao ya A na B zicheze ili kupata moja itakayoungana na AFC ya Arusha na Manyoni SC ya Singida kushuka daraja.
AFC na Manyoni tayari zimeshuka kutokana na kushindwa kucheza mechi zao za ligi hiyo katika hatua ya makundi. Kwa mujibu wa Kanuni ya 4 ya Ligi Daraja la Kwanza timu tatu zitashuka daraja.
0 maoni:
Post a Comment