Kocha Charles Boniface Mkwasa wa Twiga Stars amemuongeza mshambuliaji Rehema Salum wa Shule ya Sekondari Lord Baden ya mkoani Pwani kwenye kikosi hicho kitakachoingia kambini Machi 25 mwaka huu.
Rehema aliibuka mfungaji bora kwenye mashindano maalumu ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyoshirikisha shule nane za sekondari za Mkoa wa Dar es Salaam na kuhitimishwa Machi 8 mwaka huu.
Twiga Stars itaingia kambini kwenye kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) iliyoko Ruvu mkoani Pwani ikiwa ni sehemu ya maandalizi kwa ajili ya mechi ya mchujo ya Fainali za Wanawake Afrika (AWC) zitakazofanyika Novemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea.
Timu hiyo itacheza na Ethiopia kusaka tiketi ya kwenda Equatorial Guinea ikianzia ugenini Addis Ababa kwa mechi itakayochezwa Mei 26 mwaka huu. Timu hizo zitarudiana wiki mbili baadaye jijini Dar es Salaam.
Katika raundi ya kwanza, Twiga Stars iliitoa Namibia kwa jumla ya mabao 7-2. Ilishinda ugenini 2-0 na kuibuka na ushindi mnono nyumbani wa mabao 5-2.
Machi 10 mwaka huu, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara alizindua akaunti ya Twiga Stars kupitia Tigo Pesa kuichangia timu hiyo ili ishiriki vyema michuano ya AWC.
Wachangiaji wa Twiga Stars wanatakiwa kutuma mchango wao kwenda namba 13389 ambapo kiwango cha juu kinachoweza kutumwa kwa muhamala (transaction) mmoja ni sh. 500,000. Katika uzinduzi huo, Waziri Dk. Mukangara alichangia sh. milioni moja.
0 maoni:
Post a Comment