Thursday, March 22, 2012

MOROGORO YATAKIWA KUKAMILISHA UENYEJI

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limekipa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro (MRFA) hadi Machi 26 mwaka huu kukamilisha malipo ya sh. milioni 25 ili kuthibitisha uenyeji wake kwa Fainali ya Tisa Bora ya Ligi Daraja la Kwanza.

MRFA imeshatanguliza malipo ya sh. milioni 10 kati ya hizo kwa ajili ya kupata kituo cha fainali ambayo itatoa timu tatu zitakazocheza Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2012/2013.

Kwa hatua hiyo bado mikoa mingine iliyoomba kuwa wenyeji kupitia vyama vyao vya mpira wa miguu ina fursa ya kuandaa fainali hizo ikiwa itatimiza masharti yaliyowekwa ikiwemo kulipa kiasi hicho cha fedha (sh. milioni 25).

 Kamati ya Ligi ya TFF itakutana baada ya Machi 26 mwaka huu ili kufanya uamuzi wa mwisho wa kituo cha fainali hizo zitakazoshirikisha timu tisa.

 Timu zilizofuzu kucheza fainali hizo ni  Polisi ya Dar es Salaam, Mgambo Shooting ya Tanga, Transit Camp ya Dar es Salaam, Mbeya City Council, Mlale JKT ya Ruvuma, Tanzania Prisons ya Mbeya, Polisi ya Tabora, Polisi ya Morogoro na Rhino Rangers ya Tabora. Mikoa ambayo ilikuwa imeomba tangu awali kuwa mwenyeji wa fainali hizo zilizopangwa kuanza Machi 31 mwaka huu ni Mbeya, Morogoro, Mwanza, Ruvuma na Tabora. TFF iliiandikia mikoa yote kupitia vyama vya mpira wa miguu ikieleza masharti ya kuwa mwenyeji wa fainali hizo.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU