Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF, kwa kutumia mamlaka aliyopewa na Kanuni ya 129 ya Kanuni za Adhabu za FIFA, leo tarehe 24 Machi, 2012, ameamuru kusitishwa (provisional suspension) kwa adhabu zilizotolewa na Kamati ya Ligi ya TFF kwa wachezaji wa Timu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam. Chini ya Kanuni hiyo, Mwenyekiti anayo mamlaka ya kusitisha utekelezaji wa adhabu yoyote ile pale anapoona kwamba ukiukwaji unaolalamikiwa hautaweza kupatiwa ufumbuzi wa haraka bila kuathiri haki za wale wanaokata rufani.
Usitishwaji wa adhabu hizo, ambao utadumu kwa muda wa siku 14, kuanzia tarehe ya kusitishwa huko, una nia ya kutoa fursa kwa Sekretarieti ya TFF kuwasilisha rufani ya Yanga pamoja na maelezo yanayohusiana na rufani hiyo, mbele ya Kamati ili isikilizwe na hatimaye kuitolea maamuzi.
Kamati inasisitiza kwamba adhabu zilizotolewa na mwamuzi wa mchezo huo katika dakika 90 za mchezo hazitahusika na amri hii ya kusitisha utekelezaji, na wachezaji wanaohusika na adhabu hizo za mwamuzi wataendelea kutumikia adhabu zao hadi hapo watakapomaliza au pale maamuzi mengine yatakapotolewa.
Aidha, Kamati imeelekeza kwamba TFF ifanye juhudi za kuharakisha usikilizwaji wa rufani hiyo ili kuwawezesha wachezaji waliohusika kujua hatma yao kimichezo.
Imetolewa Dar es Salaam leo tarehe 24 Machi, 2012.
Comm. (rtd) Alfred Tibaigana
Mwenyekiti wa Kamati
0 maoni:
Post a Comment