Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaendelea na mpango wake wa kuwaendeleza waamuzi watoto wa Kituo cha Kambi ya Twalipo kilichoko Mgulani jijini Dar es Salaam kwa kuwapa mafunzo zaidi na kuwatumia katika mashindano mbalimbali.
Lengo ni kuboresha uwezo wao katika kuchezesha mchezo wa mpira wa miguu na kutoa changamoto kwa vijana wadogo wengine, hasa wa shule za msingi, sekondari na wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu kuingia katika uamuzi ili kujenga kizazi kipya katika fani hiyo.
Wazo la kuwa na waamuzi watoto lilianzia kwa Meja Bakari wa kituo hicho, juhudi ambazo TFF inazipongeza na kuziunga mkono kwa kutoa mafunzo zaidi kwa wahusika. Wiki mbili zilizopita tuliwaandalia mafunzo zaidi ya kuwanoa ambayo yaliendeshwa na Mkufunzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Leslie Liunda.
TFF imeshawatumia waamuzi hao watoto katika mashindano ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Kombe la Uhai), michuano ya vijana ya Rollingstone iliyofanyika jijini Arusha na fainali za Copa Coca-Cola. Mashindano yote hayo yalifanyika mwaka jana na kiwango walichoonesha waamuzi hao kilikuwa kizuri.
Hivyo tutaendelea kuwapa mafunzo zaidi na mashindano mengine kadri tutakavyoona inafaa kwa lengo la kuwajenga na kuwaongezea ujuzi.
SITA VPL UWANJANI WIKIENDI
Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea wikiendi hii kwa mechi tatu zitakazokutanisha timu sita kwenye viwanja tofauti.
Yanga itakuwa mwenyeji wa Azam katika mechi itakayochezwa kesho (Machi 10 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Machi 11 mwaka huu kutakuwa na mechi kati ya Simba na Toto Africans ya Mwanza itakayochezwa kwenye uwanja huo huo.
Viingilio katika mechi hizo vitakuwa sh. 3,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani, sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa viti vya VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh. 15,000.
Mechi nyingine itakayochezwa Machi 11 mwaka itakuwa kati ya Polisi Dodoma na Kagera Sugar. Mechi hiyo itachezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Jumatano ya Machi 14 mwaka huu kutakuwa na mechi mbili. Simba watakuwa wageni wa Polisi Dodoma kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma wakati Yanga watakuwa wenyeji wa African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
WAZIRI KUZINDUA TIGO PESA YA TWIGA STARS
Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangala anatarajia kuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa kuchangia timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) kupitia Tigo Pesa.
Uzinduzi huo wa akaunti maalumu ya Twiga Stars kupitia mtandao wa Tigo utafanyika kesho (Machi 10 mwaka huu) saa 5 kamili asubuhi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, na unafanywa chini ya uratibu wa kampuni ya Edge Entertainment.
Twiga Stars iko kwenye mashindano ya Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) ambapo Mei 26 mwaka huu itacheza na Ethiopia jijini Addis Ababa.
0 maoni:
Post a Comment