Thursday, April 19, 2012

25 TWIGA STARS KAMBINI APRILI 20

Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Charles Boniface Mkwasa ameita wachezaji 25 watakaoingia kambini kesho (Aprili 20 mwaka huu) kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Zimbabwe inayotarajiwa kuchezwa Aprili 28 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Mechi hiyo ni sehemu ya maandalizi ya Twiga Stars kabla ya mechi ya mashindano ya Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya Ethiopia itakayochezwa Mei 26 mwaka huu jijini Addis Ababa kabla ya timu hizo kurudiana jijini Dar es Salaam wiki mbili baadaye.

Baada ya kuripoti kambini jioni, wachezaji hao watafanyiwa vipimo vya afya (medical examination) siku inayofuata (Aprili 21 mwaka huu) na kuanza mazoezi Aprili 22 mwaka huu. Kambi ya timu hizo itakuwa kwenye hosteli za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ya Ruvu mkoani Pwani.

Wachezaji walioitwa ni Amina Ally kutoka Sekondari ya Lord Baden, Asha Rashid, Aziza Mwadini (New Generation, Zanzibar), Etoe Mlenzi (JKT Mbweni), Evelyne Sekikuto (Mburahati Queens), Fadhila Hamad (Uzuri Queens), Fatuma Bashiri (Simba Queens), Fatuma Khatib (Mburahati Queens) na Fatuma Mustafa (Sayari).

Wengine ni Fatuma Omari (Sayari), Hanifa Idd (Uzuri Queens), Maimuna Said (JKT Mbweni), Mariam Aziz (Tanzanite), Mwajuma Abdallah (Tanzanite), Mwanahamisi Omari (Mburahati Queens), Mwanaidi Tamba (Mburahati Queens), Mwapewa Mtumwa (Sayari) na Rehema Abdul (Lord Baden).

Kikosi hicho pia kina akina Rukia Khamis (Sayari), Semeni Abeid (Tanzanite), Siajabu Hassan (Evergreen), Sophia Mwasikili (Luleburgaz Spor Kulubu, Uturuki), Veneranda Mtamo (Tanzanite), Zena Khamis (Mburahati Queens) na Zena Said (Uzuri Queens).

KUONA NGORONGORO HEROES, SUDAN 3,000/-
Kiingilio cha chini cha mechi ya kuwania kucheza Fainali za Afrika kwa vijana chini ya miaka 20 kati ya Tanzania (Ngorongoro Heroes) na Sudan itakayochezwa Jumamosi (Aprili 21 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni sh. 3,000.

Mechi hiyo itaanza saa 10 kamili jioni, na viingilio vingine vitakuwa sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP C na B wakati VIP itakuwa ni sh. 15,000.

Sudan inatarajia kuwasili leo mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines ikiwa na msafara wa watu 30 na itafikia hoteli ya Rungwe iliyoko maeneo ya Kariakoo jijini Dar es Salaam. Jioni itafanya mazoezi Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.

Ngorongoro Heroes tayari iko kambini chini ya Kocha Kim Poulsen, na leo inaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Sudan yenyewe itafanya mazoezi kwenye uwanja huo kesho.

Kesho (Aprili 20 mwaka huu) saa 4 asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutakuwa na mkutano kati ya makocha wa timu zote mbili na Waandishi wa Habari.

MKUTANO MKUU TFF APRILI 21, 22
Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) utafanyika kwa siku mbili (Aprili 21 na 22 mwaka huu) kwenye ukumbi wa NSSF Waterfront jijini Dar es Salaam.

Wajumbe wa mkutano huo watawasili jijini kesho (Aprili 20 mwaka huu) na watafikia kwenye hoteli ya Royal Valentino. Wajumbe wanatoka katika vyama vya mpira wa miguu vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu ya Vodacom.

Mkutano huo utakaoanza saa 3 asubuhi utakuwa na ajenda kumi na moja. Baadhi ya ajenda hizo ni hotuba ya Rais wa TFF, taarifa ya utendaji ya mwaka 2011, bajeti ya mwaka 2012 na taarifa ya ukaguzi wa hesabu (audited accounts).

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU