Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeipa Coastal Union ushindi wa pointi tatu na mabao matatu baada ya Yanga kumchezesha mchezaji Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kwenye mechi kati ya timu hizo iliyochezwa Machi 31 mwaka huu Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Uamuzi huo ulifanywa na Kamati ya Ligi iliyokutana jana (Aprili 2 mwaka huu) kupitia ripoti mbalimbali za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza umezingatia Kanuni ya 25(f) ya Ligi Kuu ya Vodacom juu ya Udhibiti wa Wachezaji.
Kanuni hiyo inasema: “Ni lazima kwa klabu na wachezaji kutunza kumbukumbu za kadi. Klabu itakayomchezesha mchezaji mwenye kadi tatu (3) za njano au kadi nyekundu itapoteza mchezo na timu pinzani itapewa ushindi wa pointi tatu (3) na mabao matatu (3), iwapo mchezaji atacheza akiwa haruhusiwi kucheza kwa ajili ya kadi tatu (3) za njano au kadi nyekundu timu yake itapoteza mchezo. Endapo klabu haina uhakika au inataka taarifa ya idadi ya kadi zake itaomba kwa maandishi toka TFF.”
Cannavaro alioneshwa kadi nyekundu kwa kosa la kupiga kwenye mechi kati ya Yanga na Azam iliyochezwa Machi 10 mwaka huu ambapo kwa mujibu wa Kanuni ya 25(c) ya Ligi hiyo anastahili kukosa mechi tatu. Mchezaji amekosa mechi mbili tu.
Pia klabu za Coastal Union na Yanga zimepigwa faini ya sh. 500,000 kila moja kwa washabiki wake kutupa chupa za majini uwanjani wakati wa mechi hiyo. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 32(1).
Kamati ya Ligi pia imemuondoa Kamishna wa mechi hiyo Jimmy Lengwe kwenye orodha ya waamuzi kutokana na upungufu uliopo kwenye ripoti yake ambapo baadhi ya matukio makubwa hakuyaripoti. Moja ya matukio hayo ni kocha wa Coastal Union, Jamhuri Kihwelo kuzozana na mshambuliaji wa Yanga, Hamis Kiiza.
Vilevile waamuzi wa mechi namba 151 kati ya African Lyon na Simba wameandikiwa barua ya onyo kwa kupata alama za chini. Waamuzi hao ni Hashim Abdallah, Abdallah Selega, Hamis Chang’walu na Hassan Mwinchum. Naye Kamishna wa mechi namba 153 kati ya Moro United na Villa Squad, Arthur Mambeta amepewa onyo kutokana na upungufu katika ripoti yake.
0 maoni:
Post a Comment