Thursday, May 24, 2012

MALAWI YATUA KUIVAA TAIFA STARS

Timu ya Taifa ya Malawi (The Flames) inatarajiwa kuwasili nchini leo saa 10 jioni kwa ndege ya Air Malawi kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Taifa Stars itakayofanyika Jumamosi (Mei 26 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.

Mechi hiyo ni kwa ajili ya kuipima nguvu Taifa Stars kabla ya mechi yake mchujo ya Kombe la Dunia Kanda ya Afrika dhidi ya Ivory Coast itakayofanyika Juni 2 mwaka huu jijini Abidjan. Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager tayari iko kambini chini ya Kocha Kim Poulsen.

Malawi itafikia hoteli ya Sapphire iliyoko Mtaa wa Lindi na Sikukuu ambapo Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 3,000 kwa viti vya bluu na kijani, sh. 5,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 VIP B na C wakati VIP A itakuwa sh. 20,000.

Malawi ambayo itafikia hoteli ya Sapphire iliyoko Mtaa wa Lindi na Sikukuu baada ya mechi hiyo itakwenda Zanzibar ambapo Mei 28 mwaka huu itacheza na Zanzibar Heroes.

Makocha wa timu zote mbili Taifa Stars na The Flames kesho (Mei 25 mwaka huu) saa 5 asubuhi watakuwa na mkutano na waandishi wa habari kwenye ofisi za TFF.

LIGI YA TAIFA KUANZA MEI 27
Ligi ya Taifa inayoshirikisha mabingwa wa mikoa sasa itaanza Mei 27 mwaka huu badala ya Mei 26 mwaka huu kama ilivyokuwa imepangwa awali. Uamuzi wa kusogeza mbele kwa siku kuanza kwa ligi hiyo uliofanywa na Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana jana (Mei 23 mwaka huu).

Timu 23 zitachuana katika kinyang’anyiro hicho kitakachofanyika katika vituo vya Kigoma (Uwanja wa Lake Tanganyika), Musoma (Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume) na Mtwara (Uwanja wa Umoja) ambapo kinatarajia kumalizika Juni 13 mwaka huu.

Kituo cha Kigoma kina timu za Aston Villa ya Singida, Bandari (Kagera), CDA (Dodoma), JKT Kanembwa (Kigoma), Majimaji (Tabora), Mwadui (Shinyanga) na Pamba (Mwanza).

Ashanti United ya Ilala, Flamingo (Arusha), Forest (Kilimanjaro), Korogwe United (Tanga), Nangwa VTC (Manyara), Polisi (Mara), Red Coast (Kinondoni) na Tessema ya Temeke ziko kituo cha Musoma.

Kituo cha Mtwara kina timu za Kurugenzi ya Iringa, Lindi SC (Lindi), Mighty Elephant (Ruvuma), Mkamba Rangers (Morogoro), Mpanda Stars (Rukwa), Ndanda (Mtwara), Super Star (Pwani) na Tenende (Mbeya).

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU