Sunday, May 13, 2012

MANCHESTER CITY BINGWA LIGI YA ENGLAND

Manchester City ikifunga mabao mawili zikiwa zimesalia dakika mbili za nyongeza mpira kumalizika, wamefanikiwa kuunyakua ubingwa wa Ligi Kuu ya Kandanda ya England kwa kuwalaza QPR waliocheza wakiwa 10 kwa mabao 3-2 katika mchezo uliomalioza msimu kwa mtindo wa kusisimua.

Pablo Zabaleta alikuwa wa kwanza kuipatia bao la kuongoza Manchester City kabla Joleon Lescott kufanya makosa na kumpatia nafasi Djibril Cisse kuisawazishia QPR.
Joey Barton alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kukwaruzana na Carlos Tevez lakini alikuwa Jamie Mackie aliyeipatia bao la pili QPR kipindi cha pili.

Huku Manchester United ikiwa imeshailaza Sunderland, Manchester City walionekana kama wangepoteza nafasi ya kuunyakua ubingwa lakini Edin Dzeko akafanikiwa kufunga bao la kusawazisha kwa kichwa na dakika moja baadae Sergio Aguero akapachika bao la ushindi lililoimaliza kabisa QPR.

Hili ni taji la kwanza la Manchester City tangu waliposhinda kombe la Ubingwa wa Ligi daraja la kwanza wakati huo mwaka 1968.

Manchester United imepoteza taji lake la Ligi Kuu ya England, licha ya kuilaza Sunderland baada ya mahasimu wao wakubwa Manchester City kuilaza Queens Park Rangers.

Bao la kichwa lililowekwa kimiani na Wayne Rooney lilioneka kama lingempatia Sir Alex Ferguson ubingwa wa Ligi Kuu ya Kandanda kwa mara ya 13 kwa kipindi chake cha umeneja kwa miaka 20.

Manchester United walikuwa wanadhani wameshinda ubingwa baada ya Manchester City kuwa nyuma kwa mabao 2-1 na zikiwa zinaelekea dakika za nyongeza kumalizika huku mashabiki wao wakianza sherehe za ubingwa.

Lakini taarifa zilizofika kwa mashabiki wa Manchester United kwamba Manchester City wamepachika mabao mawili ya haraka haraka dakika za mwisho ziliwanyamazisha mashabiki hao na wachezaji wao wakaonekana hawaamini wanachokisikia.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU