Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga ametangaza kuwa Mkutano Mkuu wa Wanachama utafanyika Julai 15 mwaka huu ili kila Mtu atoe dukuduku lake.
Baada ya kichapo cha bao 5-0 toka kwa Mahasimu wao Simba Jumapili kwenye Mechi ya mwisho ya Msimu ya Ligi Kuu Vodacom, Yanga imekuwa ikigubikwa na vuta nikuvute ya vikundi mbalimbali ambavyo vimerundikana Makao Makuu ya Klabu hiyo Mtaa wa Jangwani Jijini Dar es Salaam na kusababisha Polisi kuweka ulinzi imara.
Akizungumza na Wanahabari hapo Makao Makuu, Nchunga alisema amesikitishwa na wao kushindwa kutetea Ubingwa wao lakini amewataka Wana Yanga wote wajipange upya.
Na ili kuimarisha umoja na mshikamano na pia kubadilishana mawazo na uzoefu, Uongozi wake Nchunga umepanga kukutana na Makundi mbalimbali na kuanzia kesho watakutana na Wazee wa Yanga.
Pia Nchunga alichambua sababu za kutofanya vizuri kwenye Ligi Msimu huu na kumaliza nafasi ya 3 na alitaja kuwa ni pamoja mabadiliko ya Benchi la Ufundi ambapo walianza na Kocha toka Uganda Sam Timbe na baadae kumwondoa na kumpachika Mserbia Kostadin Papic.
Nchunga aliwasisitiza Wanachama kulipa Ada zao ili wapate nafasi kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Julai 15.
0 maoni:
Post a Comment