TFF KUZAWADIA WAPIGA PICHA COPA COCA-COLA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litawazawadia wapiga picha za magazetini watakaoripoti mashindano ya Copa Coca-Cola 2012 ngazi ya Taifa yanayoendelea kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Mashindano hayo yanayodhaminiwa na Kampuni ya Coca-Cola na kushirikisha mikoa 28 yanafanyika viwanja vya Tanganyika Packers, Kumbukumbu ya Karume mkoani Dar es Salaam, na viwanja vya Tamco na Nyumbu mkoani.
Zawadi ya sh. 250,000 itatolewa kwa picha bora katika maeneo matatu; action picture, fair play picture na mpiga picha ambaye ameripoti matukio mengi ya mashindano hayo yanayoshirikisha vijana wenye umri chini ya miaka 17.
Washiriki wanatakiwa kuwasilisha picha zao zilizotumika (cuttings) ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
MABINGWA COPA WALALA KWA RUVUMA
Ruvuma imeanza vizuri michuano ya Copa Coca-Cola baada ya kuwafunga mabingwa watetezi Kigoma mabao 2-0 katika mchezo wa kundi A uliofanyika leo asubuhi (Juni 26 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
Kigoma ambayo iliifunga Lindi mabao 2-0 katika mechi ya ufunguzi iliyochezwa juzi, ilishindwa kufua dafu mbele ya Ruvuma na kuruhusu bao katika kila kipindi.
Mabao yote ya washindi yalifungwa na mshambuliaji Edward Songo. Mshambuliaji huyo alifunga bao la kwanza dakika ya 34 wakati la pili alilipachika dakika ya 84.
Katika mechi nyingine zilizochezwa leo asubuhi, Tanga na Morogoro zilitoka sare ya mabao 3-3 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Tanganyika Packers ulioko Kawe, Dar es Salaam.
Mkoani Pwani, Mara iliifunga Temeke bao 1-0 kwenye Uwanja wa Nyumbu wakati Kagera ililala bao 1-0 mbele ya Kilimanjaro katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Tamco.
0 maoni:
Post a Comment