Timu 10 za Tanzania Bara zitashiriki kwenye michuano ya Rollingstone kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 ambayo mwaka huu itafanyika Makamba nchini Burundi kuanzia Julai 7 mwaka huu.
Jumla ya timu 24 zinashiriki mashindano hayo na zimepangwa katika makundi sita tofauti. Timu nyingine zinatoka Burundi, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Uganda na Zanzibar.
Timu za Tanzania zilizoingia katika mashindano hayo ni Azam, Bishop High School, Chakyi Academy, Coastal Union, Rollingstone, Ruvu Shooting, Simba, TAYFA Academy, Yanga na Young Life.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Rollingstone, Issa Karata timu zote zinatakiwa kwenda vyeti vya kuzaliwa vya wachezaji wake ili kuthibitisha umri wao. Kamati ya Mashindano itakuwa na uamuzi wa mwisho kuhusu umri wa mchezaji yeyote.
Kila timu inatakiwa kuwa na wachezaji 20 na viongozi watano ambao watagharamiwa na waandaaji kwa huduma za malazi na chakula kwa muda wote wa mashindano hayo yaliyoanzishwa miaka 13 iliyopita.
MCHAKATO UCHAGUZI DRFA KUANZA JULAI 15
Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeridhia ombi la Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kuanza mchakato wa uchaguzi wake Julai 15 mwaka huu.
DRFA iliwasilisha ombi TFF ili kusogeza mbele kuanza kwa mchakato huo kwa vile Katiba yao ambayo waliagizwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuifanyia marekebisho kabla ya kuingia kwenye uchaguzi huo bado iko kwa Msajili.
Awali DRFA ilikuwa ianze mchakato wa uchaguzi Julai Mosi mwaka huu. Kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF, mchakato wa uchaguzi unatakiwa kuchukua siku 40 tangu kuanza kutolewa fomu kwa wagombea hadi siku yenyewe ya uchaguzi.
Pia Kamati ya Uchaguzi ya TFF imekubali ombi la Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Kigoma (KRFA) kuanza mapema mchakato wa uchaguzi wake. Sasa mchakato wa uchaguzi wa chama hicho utaanza Septemba Mosi mwaka huu badala ya Septemba 15 mwaka huu kama ilivyokuwa imepangwa awali.






0 maoni:
Post a Comment