Tuesday, July 3, 2012

WAKENYA KUICHEZESHA NGORONGORO HEROES NYUMBANI


Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Kenya kuchezesha mechi ya raundi ya pili kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 kati ya Tanzania (Ngorongoro Heroes) na Nigeria.

Mwamuzi atakayechezesha mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili itakayofanyika Julai 29 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam atakuwa Moses Ojwang Osano.

Waamuzi wasaidizi watakuwa Peter Keireini na Elias Kuloba Wamalwa wakati mwamuzi wa mezani (fourth official) ni Thomas Onyango. Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Charles Masembe kutoka Uganda.

Pia CAF imemteua Alfred Kishongole Rwiza wa Tanzania kuwa Kamishna wa mechi ya michuano hiyo kati ya Misri na Kenya itakayochezwa jijini Cairo kati ya Julai 27, 28 na 29 mwaka huu.

TEMEKE YAICHAPA DODOMA 2-0 COPA
Temeke imefainikiwa kuilaza Dodoma mabao 2-0 katika mechi ya kundi C ya michuano ya Copa Coca-Cola iliyochezwa leo (Julai 3 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Tanganyika Packers ulioko Kawe, Dar es Salaam.

Mabao ya washindi ambao kwa matokeo hayo sasa wamefikisha pointi tano yalifungwa dakika ya tano Hassan Kabunda wakati la pili lilifungwa dakika ya 34 na Abdul Hassan.

Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam umeshuhudia Morogoro ikiibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Iringa lililofungwa dakika ya 37 na Mutalemwa Katunzi.

Nayo Kilimanjaro imeibuka na ushindi wa bao 1- dhidi ya Tabora katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Nyumbu mkoani Pwani. Bao hilo katika mechi hiyo ya kundi D lilifungwa dakika ya 14 na Eric Christopher.

Kwa matokeo hayo Tabora imebaki na pointi tatu baada ya kushinda mechi moja tu dhidi ya Pwani, na imebakiza mechi moja dhidi ya Kusini Unguja ambayo hata ikishinda haiwezi kuingia hatua ya 16 bora.

Nao mabingwa watetezi Kigoma wamejiweka katika nafasi nzuri ya kucheza 16 bora baada ya kuitandika Kusini Pemba mabao 3-1 katika mchezo wa kundi A uliochezwa Uwanja wa Tamco ulioko mkoani Pwani

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU