Sunday, July 22, 2012

UCHAGUZI WA VIONGOZI WA NETIBOLI KUFANYIKA AGOSTI 11,2012

CHAMA cha Netiboli Mkoa wa Dar es Salaam (CHANEDA), kinatarajia kufanya uchaguzi wa viongozi wake Agosti 11, mwaka huu jijini.



 Ofisa Habari wa CHANEDA, Michael Maurus, alisema kuwa uchaguzi huo unafanyika, ikiwa ni baada ya viongozi waliopo madarakani kumaliza muda wao tangu mwaka jana.

Alisema kuwa kuchelewa kufanyika kwa uchaguzi huo kulitokana na vyama vya wilaya za Ilala, Kinondoni na Temeke kutofanya chaguzi zao ili kupata wapiga kura halali ambao ndio watakaochagua viongozi wa mkoa.

“Ili uchaguzi ufanyike, lazima kuwapo na wapiga kula halali ambao ni viongozi wa klabu na vyama vya netiboli vya wilaya, tuliagiza vyama vifanye chaguzi, lakini hadi sasa hakuna mwitikio wowote, hivyo tumeona tuwatumie viongozi wa klabu kufanya uchaguzi huo wa mkoa ili viongozi watakaopatikana wapange taratibu za kufuatilia kila chama cha wilaya kuona nini kinaendelea huko,” alisema Maurus.

Juu ya uchaguzi huo wa CHANEDA, Maurus alisema kuwa mchakato wa uchukuaji fomu na kurudisha, unaanza Jumatatu ya Julai 23 hadi Julai 30, mwaka huu wakati usaili itakuwa ni Agosti 4, mwaka huu.

Maurus alisema kuwa fomu za kuwania uongozi huo zinapatikana katika ofisi ya Ofisa Michezo Mkoa wa Dar es Salaam.

Kwa sasa viongozi waliobaki wanaokisimamia chama hicho ni Mwenyekiti Winfida Emmanuel, Katibu Mkuu Joseph Ng’anza na Maurus akiwa kama Ofisa Habari na Katibu Msaidizi.

Wengine waliokuwa na nafasi CHANEDA ambao hata hivyo hawakuwa karibu na chama hicho kutokana na sababu mbalimbali, ni Jackson Henzron (Mweka Hazina), Christina Kimamla, Mussa Sambala, Khadija Ally na Moshi Mganga (wote wajumbe), huku Makamu Mwenyekiti akiwa ni Pili Mogella ambaye hata hivyo alijiondoa kutokana na kutohudhuria vikao.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU