Wednesday, September 26, 2012

KAMATI YA UCHAGUZI TFF YATUPA RUFANI YA WARUFANI IRFA

 Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ilikutana jana (Septemba 25 mwaka huu) kusikiliza rufani iliyowasilishwa mbele yake na warufani Mussa H. Mahundi, Abou O. Sillia na Alex Mgongolwa dhidi ya Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Iringa (IRFA) iliyoomba Kamati ya Uchaguzi ya TFF kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa IRFA uliofanyika Septemba 8 mwaka huu Mufindi, Iringa, na kuomba uchaguzi huo ufanyike upya kwa kuendeshwa na kusimamiwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
 
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Deogratias Lyatto, baada ya kupitia maelezo ya warufani na warufaniwa, Kamati ya Uchaguzi ya TFF imejiridhisha kuwa rufani iliyowasilishwa mbele yake na Mahundi, Sillia na Mgongolwa ilikosa sifa ya kuwa rufani kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF, Ibara ya 8(2), Ibara ya 21(3) na 24(2). Kwa kutozingatia matakwa ya Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF, Kamati ya Uchaguzi ya TFF imetupa rufani hiyo.
 
Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeiagiza Kamati ya Uchaguzi ya IRFA kuchukua hatua dhidi ya Abuu Changawa kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF, Ibara ya 28(6) kwa kuingilia mchakato wa uchaguzi wa IRFA siku ya uchaguzi.
 
SHUKRANI KWA WADAU SERENGETI BOYS
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linawashukuru wadau waliofanikisha kwa njia mbalimbali ziara ya timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) iliyofanyika hivi karibuni katika mikoa ya Mbeya na Njombe.
 
Wadau hao ni Chama cha Mpira wa Miguu Mbeya Mjini (MUFA) chini ya Mwenyekiti wake Suleiman Haroub, Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Njombe (NJOREFA), Stanley Lugenge, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya (MREFA) na Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Njombe (NDFA).
Wengine ni Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Makambako (MDFA), Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro (MRFA), na klabu za Mbozi United, Kyela United, Tanzania Prisons na Mbeya City.
 
Serengeti Boys inaendelea na kambi yake jijini Dar es Salaam kujiandaa kwa mechi ya kwanza ya mchujo ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 dhidi ya Misri itakayochezwa Oktoba 14 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
 

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU