Friday, September 21, 2012

MUDA WA MECHI ZA ‘LIVE’ SUPER WEEKEND

Mechi tano za Ligi Kuu ya Vodacom za Super Weekend katika mzunguko wa kwanza zitakazooneshwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha Super Sport zitaanza kati ya saa 1-.30 jioni na saa 1 kamili usiku.
Septemba 28 mwaka huu kutakuwa na mechi kati ya Azam na JKT Ruvu itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 1 kamili usiku. Mechi ya Simba na Tanzania Prisons itakayochezwa Septemba 29 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam itaanza saa 11 kamili jioni.
Yanga na African Lyon zenyewe zitapambana Septemba 30 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 11 kamili jioni wakati Ruvu Shooting na Mtibwa Sugar zitaoneshana kazi Oktoba 1 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kuanzia saa 10.30 jioni.
Mechi ya mwisho katika Super Weekend itakuwa Oktoba 3 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikiwakutanisha watani wa jadi Yanga na Simba, na itaanza kutimua vumbi saa 1 kamili usiku.
TWFA YATANGAZA KAMATI YA UCHAGUZI
Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) kimetangaza Kamati ya Uchaguzi yenye wajumbe watano kwa ajili ya uchaguzi wake unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu.
Kaimu Mwenyekiti wa TWFA, Margreth Mtaki amewaambia Waandishi wa Habari, Dar es Salaam leo kuwa kamati hiyo itaongozwa na Ombeni Zavala, na itarajia kutangaza mchakato wa uchaguzi huo Jumatatu (Septemba 24 mwaka huu).
Aliwataja wajumbe wengine wa kamati hiyo yenye jukumu la kuendesha uchaguzi wa chama hicho kuwa ni Rachel Masamu, Lloyd Nchunga, Nancy Mabula na Maneno Tamba.
Pia aliwataka wadau wa mpira wa miguu wa wanawake kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika TWFA mara Kamati ya Uchaguzi itakapoanza mchakato.
Wakati huo huo, uchaguzi wa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa ya Kilimanjaro (KRFA) na Manyara (MARFA) unafanyika kesho (Septemba 22 mwaka huu).

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU