MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara,
Simba, wameendeleza wimbi la ushindi wa asilimia 100, baada ya kuibuika na
ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting, pambano lililochezwa leo kwenye Uwanja
wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Simba ilipata bao la kuongoza dakika ya 30, likiwekwa
nyavuni na nyota wa kimataifa wa Zambia, Sunzu kwa kichwa maridadi akimalizia
krosi iliyopigwa baada ya kazi nzuri ya kuwachambua mabeki iliyofanya na Said
Nassor ‘Cholo’ aliyepanda kusaidia mashambulizi.
Dakika 38, Kiemba akawachachafya wachezaji wa Ruvu, kabla ya
krosi yake kukosa mmaliziaji na kuishia mikononi mwa Benjamin Haule.
Simba iliendelea kushambulia ambapo katika dakika ya 44, beki Mau
Bofu wa Ruvu alimwangusha Sunzu ndani ya 18 na mwamuzi Swai kuamuru ipigwe penati. Akuffor
akabeba jukumu la kupiga tuta hilo, ambalo mlinda mlango Haule alipangua na
kuwa kona tasa.
Hadi mapumziko, Simba ilitoka ikiongoza kwa bao hilo, huku
mashabiki waliohudhuria mechi hiyo wakishuhudia maamuzi tata ya mwamuzi Swai,
aliyeonekana dhahiri kutowajali vibendera wake Samwel Mpenzu na Godfrey Kihwili
wote wa Arusha pindi wanapoashiria madhambi.
Kipindi cha pili kilianza kwa Ruvu kushambulia lango la
Wekundu na kama si umakini mdogo miongoni mwa washambuliaji wake Paul Ndauka,
Hussein Said na Hassan Dilunga aliyekuwa akipenya kirahisi safu ya ulinzi,
wangeweza kupata mabao.
Sunzu akafanya shambuliazi kali dakika ya 55 lililotokana na
jitihada binafsi akiwalima chenga mabeki, kabla ya Ruvu nao kurudi langoni mwa
Simba na Dilunga (Hassani) nusura aipatie bao timu yake, kabla ya mawasiliano
madogo na Abdulrahman Mussa kumgharimu.
Ruvu ikapata bao la kusawazisha mnamo dakika ya 78,
lililowekwa nyavuni na mtokea benchi Seif Rashid, akitumia makosa ya beki Juma
Nyoso wa Simba, aliyeshindwa kuondoa hatari langoni akiwa peke yake na
kuukanyaga mpira huo na kuteleza, ambapo Seif aliunasa na kumchambua Juma
Kaseja.
Wakati wengi wakimiani matokeo ya pambano hilo yangebaki
kuwa ni sare ya bao 1-1, mtokea benchi wa Simba, Christopher Edward aliyeingia
kuchukua nafasi ya Akuffor, akaipatia timu yake bao la pili dakika ya 87 kwa
shuti na kuamsha mamia ya mashabiki wake jukwaani.
0 maoni:
Post a Comment