Azam
ya Dar es Salaam na Coastal Union ya Tanga ndizo zitakazoumana kwenye
fainali ya michuano ya Kombe la Uhai 2012 itakayochezwa kesho jioni
(Desemba 23 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es
Salaam.
Timu
hizo zimepata fursa hiyo baada ya kushinda mechi zao za nusu fainali ya
michuano hiyo inayoshirikisha timu za vijana wenye umri chini ya miaka
20 za klabu za Ligi Kuu ya Vodacom. Michuano hiyo inayodhaminiwa na
kampuni ya Said Salim Bakhresa kupitia maji Uhai.
Azam
ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata tiketi ya fainali baada ya kuitoa
Mtibwa Sugar ya Morogoro kwa mikwaju ya penalti 3-2. Matokeo ya dakika
90 yalikuwa bao 1-1. Nayo Coastal Union iliivua ubingwa Simba kwa
kuifunga mabao 2-1.
Mechi
ya fainali itaanza saa 10 kamili jioni, na itatanguliwa na ile ya
kutafuta mshindi wa tatu kati ya Mtibwa Sugar na Simba ambayo itachezwa
saa 2 kamili asubuhi kwenye uwanja huo huo.
Mbali
ya kombe, bingwa wa michuano hiyo atapata sh. milioni 1.5, makamu
bingwa sh. milioni 1 wakati mshindi wa tatu atajinyakulia sh. 500,000.
Timu iliyoonesha zaidi mchezo wa kiungwana (fair play) itapata sh.
400,000, mchezaji bora wa mashindano sh. 350,000, mfungaji bora sh.
300,000 na kipa bora sh. 300,000.
Naye kocha bora katika mashindano hayo atazawadiwa sh. 300,000 kama itakavyokuwa kwa refa bora.
0 maoni:
Post a Comment