(A)
Msama yapiga jeki mkutano TASWA
KAMPUNI ya Msama Promotions inayoandaa
Tamasha la Pasaka imeahidi kutoa Sh. Milioni 1.5 kwa ajili ya Mkutano Mkuu wa
Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) utakaofanyika Bagamoyo mkoani Pwani wiki ijayo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya
tamasha hilo, Alex Msama ambaye ndiye Mkurugenzi wa kampuni hiyo amesema
ushirikiano wake na wanahabari
umemsukuma kusaidia kiasi hicho cha fedha.
Msama ameahidi kuendelea kushirikiana na
TASWA kadri awezavyo na kwamba mafanikio ya Tamasha la Pasaka yanachangiwa kwa
kiasi kikubwa na wanahabari.
“Kampuni yangu ya Msama Promotions kupitia
Tamasha la Pasaka tumeamua kuungana na wanahabari katika kufanikisha mkutano
wenu, tunaamini uhusiano wetu utaendelea kuwa wa kupigiwa mfano,” ilisema
sehemu ya taarifa ya TASWA jana ikimkariri Msama.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa TASWA, Amir
Mhando alishukuru kwa udhamini huo na kuomba wengine wenye moyo wajitokeze
kuwasaidia kwani bajeti yao ni Sh. Milioni 20. Tayari kampuni ya simu za
mkononi ya Zantel imeshatangaza udhamini wa Sh. Milioni sita.
Mhando alisema maandalizi ya Mkutano Mkuu wa
TASWA utakaofanyika wiki ijayo Bagamoyo mkoani Pwani yanaendelea vizuri na
kwamba zaidi ya wanachama 100 wa TASWA na wadau wengine wa TASWA wamethibitisha
kushiriki.
(B)
Pongezi
Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo
Tanzania (TASWA), kinatoa pongezi kwa wanachama wake Benny Kisaka na Zena
Chande kwa kufanikiwa kuwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF).
Kisaka alishinda wadhida huo wiki iliyopita
kupitia uchaguzi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), wakati Chande
alishika Jumatano katika uchaguzi wa Chama cha Mpira wa Miguu Wanawake Tanzania
(TWFA).
Tunaamini wajumbe wa Mkutano Mkuu DRFA na wale wa TWFA
hawakufanya makosa, wamefanya uamuzi sahihi na wamepata watu sahihi na makini
na michango yao itakuwa yenye tija kubwa kwa maendeleo la mpira wa miguu hapa
nchini.
Tunawatakia kila la heri wanachama wetu hao
katika changamoto mbalimbali watakazokutana nazo kwenye nafasi zao hizo
walizopata.
0 maoni:
Post a Comment