Thursday, December 20, 2012

NUSU FAINALI UHAI CUP KUPIGWA KARUME

Mechi za nusu fainali ya michuano ya Kombe la Uhai 2012 inayoshirikisha timu za vijana wenye umri chini ya miaka 20 za klabu za Ligi Kuu ya Vodacom zitachezwa kesho (Desemba 21 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.

Nusu fainali ya kwanza ya michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Said Salim Bakhresa kupitia maji Uhai itazikutanisha timu za Mtibwa Sugar ya Morogoro na Azam na itafanyika kuanzia saa 2 kamili asubuhi.

Simba na Coastal Union zitacheza nusu fainali ya pili kuanzia saa 10 kamili jioni kwenye uwanja huo huo. Mtibwa Sugar imepata tiketi ya nusu fainali baada ya kuichapa African Lyon mabao 3-1 wakati Simba iliilaza Oljoro JKT mabao 2-0.

Nayo Azam iliindoa JKT Ruvu kwenye robo fainali kwa bao 1-0 huku Coastal Union ikipata ushindi wa penalti 4-3 dhidi ya Ruvu Shooting kwenye mechi ya mwisho ya robo fainali.

Mechi ya fainali na ile ya kutafuta mshindi wa tatu zitachezwa Jumapili (Desemba 23 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam. Mechi ya mshindi wa tatu itaanza saa 2 kamili asubuhi wakati ya fainali itakuwa saa 10 kamili jioni.

PONGEZI KWA UONGOZI MPYA TWFA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaupongeza uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika jana (Desemba 19 mwaka huu) hoteli ya Midlands mjini Morogoro.

Ushindi aliopata Lina Kessy aliyechaguliwa tena kuwa Mwenyekiti pamoja na wajumbe wengine wa Kamati ya Utendaji unaonesha jinsi ambavyo wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TWFA walivyo na imani kwao.

TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya TWFA, na kwamba ina changamoto kubwa ya kuhakikisha inaendesha shughuli za chama hicho kwa kuzingatia katiba na kanuni.

Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya TWFA chini ya Mama Ombeni Zavala na Kamati ya Uchaguzi ya TFF inayoongozwa na Deogratias Lyatto kwa kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa utulivu na kwa kuzingatia Katiba ya TWFA na Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.

Safu mpya ya uongozi wa DRFA inaundwa na Lina Kessy (Mwenyekiti), Rose Kissiwa (Makamu Mwenyekiti), Amina Karuma (Katibu), Zena Chande (Mwakilishi wa Mkutano Mkuu wa TFF) wakati mjumbe wa Kamati ya Utendaji ni Triphonia Temba.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU