Mpambano wa kutafuta Mfalme wa uzito wa Bantam wa Kimataifa (IBF
International Bantamweight Title) kati ya mabondia Immaneul Naidjala a.ka. Prince kutoka nchini Namibia and bondia
mwenzake Lesley Sekotswe kutoka nchini
Botswana umeanza kuleta hamasha kubwa katika nchi hii yenye wakazi wapatao milioni
mbili.
Mabondia wote wawili walikutana kwa mara nyingine tena leo
katika ofisi za Bodi ya Mieleka na Ngumi ya Namibia katika zoezi la kupima
uzito na ilibidi askari zaidi ya 15 kuwazuia wasizipige kavukavu.
Moto ulianza kuwashwa wakati bondia Lesley Sekotswe wa Botswana alipoingia katika chumba cha waandishi
wa habari na kutangaza rasmi kuwa atamshughulikia Prince Immanuel Naidjala vilivyo na asijaribu kufikiri kuwa atafika zaidi ya
raundi ya tatu.
Wakati huo Prince
Immanuel alikuwa kwenye chumba cha kupimia afya za wabondia na alikurupuka
kutaka kumwingilia Lesley kabla ya askari waliokodishwa na Promota Nestor Tobias
kuingilia kati na kuwatenganisha ili wasianze mpambano unaosubiriwa kesho.
Katika zoezi la vipimo ambalo lilisimamiwa na Rais wa IBF
katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati Mtanzania Onesmo
Ngowi, bondia Lesely Sekotswe wa Botswana alikutwa na kilo 53.45 wakati Prince
Immanuel wa Namibia alikutwa na kilo 53.35. Rais Ngowi aliwatangaza mabondia
wote kuwa katika uzito unaotakiwa.
Daktari Leonardo Perves kutoka nchini Cuba inayojulikana kwa
kutoa mabondia wengi mabingwa wa mashindano ya Olimpiki na Dunia ndiye
aliyewapima mabondia hao na kuwatangaza kuwa wana afya nzuri ya kuweza
kuzipiga.
Mpambano huu utafanyika siku moja kabla ya sherehe za uhuru
wa nchi ya Namibia katika ukumbi wa Windhoek
Country Club Resort and Casino ulioko nje kidogo mwa jiji la Windhoek na
utatanguliwa na mepambano mengine kadhaa ya utangulizi.
Katika mkutano na waandishi wa bahari Rais Ngowi aliisifu serikali
ya nchi ya Namibia kwa jinsi inavyoipa kipa umbele tasnia ya ngumi katika
juhudi zake za kuitangaza nchi na kujenga ajira kwa vijana. Ngowi aliihakikishia
nchi ya Namibia kuwa ataiingiza katika programu ya IBF ya Utalii wa Michezo (IBF Sports Tourism) ili nayo iweze
kufaidi katika maendeleo ya Utalii wa Michezo
duniani.
0 maoni:
Post a Comment