Kiingilio
cha chini katika mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Tanzania (Taifa
Stars) na Morocco (Lions of the Atlas) itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani.
Viti
vya kijani katika uwanja huo wenye uwezo wa kumeza watazamaji 60,000 viko 19,648.
Kwa upande wa viti vya rangi ya bluu ambavyo viko 17,045 ni sh. 7,000. Kiingilio
kwa viti vya rangi ya chungwa ambavyo viko 11,897 ni sh. 10,000.
Viingilio
vya daraja la juu ni kama ifuatavyo; VIP C yenye watazamaji 4,060 ni sh. 15,000
wakati sh. 20,000 ni kwa VIP B yenye watazamaji 4,160. VIP A yenye watazamaji
748 kiingilio chake ni sh. 30,000.
Tiketi
kwa ajili ya mechi hiyo itakayoanza saa 9 kamili alasiri zitaanza kuuzwa siku
mbili ya mchezo (Ijumaa na Jumamosi) katika vituo vifuatavyo; Shule ya
Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa
Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni na Dar Live Mbagala.
Katika
vituo hivyo tiketi zitauzwa katika magari maalumu. Magari hayo pia yatafanya
mauzo ya tiketi uwanjani siku ya mechi. Vilevile tunapenda kuwakumbusha
watazamaji kutonunua tiketi mikononi mwa watu au katika maeneo yasiyohusika ili
kuepuka kununua tiketi bandia, hivyo kukosa fursa ya kushuhudia mechi hiyo.
SAMATA,
ULIMWENGU WARIPOTI STARS
Washambuliaji
wa Taifa Stars, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP
Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) wamewasili nchini jana usiku
na kwenda moja kwa moja kambini.
Ujio
wa washambuliaji hao unafanya idadi ya wachezaji walioripoti kambini kufikia 20
kati ya 23 walioitwaa baada ya mshambuliaji Khamis Mcha aliyekuwa na kikosi cha
timu yake ya Azam nchini Liberia naye kuripoti kambini leo asubuhi.
Wachezaji
John Bocco na makipa Mwadini Ally na Aishi Manula ambao pia nao walikuwa
Liberia na timu yao ya Azam wataripoti kambini leo alasiri. Wachezaji hao ni
sehemu ya msafara wa timu ya Azam ambao utakuja na ndege ya mchana kutokea
Nairobi kwa vile ile ya asubuhi waliyotangulia nayo wenzao kuwa imejaa.
Taifa
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ikiwa chini ya Kocha Kim
Poulsen leo inaendelea na mazoezi Uwanja wa Taifa. Mazoezi hayo yataanza saa 9
alasiri.
TIMU TATU
ZASHUKA DARAJA FDL
Timu
tatu zimeshuka daraja kutoka Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kurudi Ligi ya Mkoa
msimu ujao wa 2013/2014 baada ya kushika nafasi za mwisho katika ligi hiyo
msimu huu 2012/2013 iliyomalizika wikiendi iliyopita.
Small
Kids ya Rukwa imeporomoka kutoka kundi A baada ya kuondolewa kwenye michuano
hiyo mapema kwa kushindwa kufika uwanjani kwenye moja ya mechi zake. Kwa mujibu
wa kanuni matokeo yote ya mechi ilizocheza yalifutwa.
Moro
United ya Dar es Salaam ndiyo iliyoaga FDL kutoka kundi B baada ya kumaliza
mechi zake ikiwa na pointi tatu. Wakati kutoka kundi C timu iliyoshuka ni
Morani ya Manyara iliyomaliza ligi ikiwa na pointi kumi na moja.
Timu
zilizopanda daraja kucheza Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2013/2014 ni Mbeya City
ya Mbeya iliyoongoza kundi A ikiwa na pointi 31, vinara wa kundi B timu ya
Ashanti United ya Dar es Salaam yenye pointi 29 wakati Rhino Rangers ya Tabora
imepanda kutoka kundi C ikiwa na pointi 32.
LIUNDA
KUTATHIMINI WAAMUZI KOMBE LA DUNIA
Mwamuzi
Msaidizi wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Leslie Liunda ameteuliwa kuwa
mtathimini wa waamuzi (referee assessor) kwenye moja ya mechi za mchujo za
Kombe la Dunia.
Shirikisho
la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limemteua Liunda kutathimini waamuzi
kwenye mechi kati ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Libya
itakayochezwa Jumapili (Machi 24 mwaka huu).
Mechi
hiyo itafanyika kwenye Uwanja wa Martyrs jijini Kinshasa kuanzia saa 9.30
alasiri kwa saa za Afrika ya Kati (CAT).
Waamuzi
watakaochezea mechi hiyo William Selorm Agbovi atakayekuwa mwamuzi wa kati,
Malik Alidu Salifu (mwamuzi msaidizi namba moja), David Laryea (mwamuzi
msaidizi namba mbili) na mwamuzi wa mezani (fourth official) Cecil Amatey
Fleischer. Waamuzi wote hao wanatoka Ghana.
0 maoni:
Post a Comment