Friday, March 15, 2013

RUVU SHOOTING KUIKABILI YANGA VPL

 
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho (Machi 16 mwaka huu) kwa mechi tatu ambapo Yanga itakuwa mgeni wa Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mwamuzi Jacob Adongo kutoka Musoma mkoani Mara ndiye aliyepewa jukumu la kuchezesha mechi hiyo namba 146. Adongo atasaidiwa na Anold Bugado wa Singida na Milambo Tshikungu kutoka Mbeya wakati mwamuzi wa mezani ni Hashim Abdallah wa Dar es Salaam.

Mtathmini wa waamuzi ni Army Sentimea wakati Kamishna wa mechi hiyo inayokutanisha vinara Yanga na Ruvu Shooting inayoshika nafasi ya saba ikiwa na pointi 29 chini ya ukufunzi wa Charles Boniface Mkwasa na Msaidizi wake Selemani Mtungwe ni Emmanuel Kavenga kutoka Mbeya.

Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 5,000 kwa viti vya bluu na kijani, sh. 8,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 kwa viti vya VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh. 20,000.

Pia TFF inawaasa washabiki wa mpira wa miguu kuacha kununua tiketi mikononi mwa watu kwa vile wanaweza kuuziwa tiketi bandia. Tiketi zote zitauzwa katika vituo vinavyotangazwa katika magari maalumu, na uwanjani pia katika magari hayo.

Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wenye uwezo wa kuchukua washabiki 25,000 utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Toto Africans na Mgambo Shooting kutoka Tanga. Ugumu wa mechi hiyo unatokana na ukweli kuwa timu zote mbili zinapigana kuepuka kurudi zilikotoka (daraja la kwanza).

Mgambo Shooting inayonolewa na Mohamed Kampira inashika nafasi ya tisa ikiwa na pointi 24 katika ligi hiyo yenye timu 14. Toto Africans ambayo iko nyumbani itaingia uwanjani ikiwa na pointi 14 katika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi.

Baada ya kulala 2-1 mbele ya Simba katika mechi iliyopita, Coastal Union itakuwa mgeni wa Mtibwa Sugar katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro.

Ligi hiyo itaendelea tena keshokutwa (Machi 17 mwaka huu) kwa mechi moja itakayozikutanisha JKT Ruvu na Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Azam Complex.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU