Sunday, March 17, 2013

WAANGOLA KUCHEZESHA MECHI YA STARS

 
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limeteua waamuzi kutoka Angola kuchezesha mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Morocco (Lions of the Atlas).

Mechi hiyo ya kundi C itachezwa Machi 24 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Ivory Coast ndiyo inayoongoza kundi hilo ikiwa na pointi nne na kufuatiwa na Taifa Stars yenye pointi tatu.

Mwamuzi wa mechi hiyo ni Helder Martins de Carvalho wakati mwamuzi msaidizi namba moja ni Inacio Manuel Candido huku Ricardo Daniel Cachicumi akiwa mwamuzi msaidizi namba mbili. Mwamuzi wa mezani (fourth official) ni Antonio Muachihuissa Caxala.

Waamuzi hao watawasili nchini saa 1.20 usiku Machi 22 mwaka huu kwa ndege ya Kenya Airways wakitokea Luanda, Angola kupitia Nairobi, Kenya.

Kamishna wa mechi hiyo atakuwa David Fani kutoka Botswana anatarajiwa kuwasili Machi 22 mwaka huu saa 1.45 usiku kwa ndege ya South African Airways.

Naye mtathmini wa waamuzi (referee assessor) Neermal Boodhoo kutoka Afrika Kusini atawasili nchini Machi 22 mwaka huu 1.45 usiku kwa ndege ya South African Airways.

TAIFA STARS YAINGIA KAMBINI KUIWINDA MOROCCO
Taifa Stars imeanza kambi jana jioni (Machi 16 mwaka huu) ambapo wachezaji 14 kati ya 23 walioitwa wameripoti na kufanya mazoezi leo asubuhi chini ya Kocha Kim Poulsen.

Wachezaji walioripoti ni nahodha Juma Kaseja kutoka Simba na msaidizi wake Aggrey Morris wa Azam, Erasto Nyoni (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga), Nassoro Masoud Cholo (Simba), Shomari Kapombe (Simba) na Salum Abubakar (Azam).

Wengine ni Athuman Idd (Yanga), Amri Kiemba (Simba), Frank Domayo (Yanga), Mwinyi Kazimoto (Simba), Mrisho Ngasa (Simba) na Simon Msuva (Yanga).

Wachezaji Hussein Shariff, Issa Rashid na Shabani Nditi ambao timu yao ya Mtibwa Sugar jana ilicheza mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) mjini Turiani wataripoti kambini leo jioni.

Kikosi hicho kitakamilika Jumanne asubuhi baada ya wachezaji walio katika kikosi cha Azam nchini Liberia kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho kurejea nchini. Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemorasi ya Congo (DRC) wanatarajiwa kutua nchini kesho usiku.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU