BENDI
ya muziki wa dansi ya Extra Bongo na kundi la taarabu la Jahazi Modern ndiyo
burudani zitakazonogesha tamasha la vyombo vya habari litakalofanyika Dar es
Salaam kesho (Jumamosi).
Akizungumza
Dar es Salaam jana, wakati wa kutambulisha burudani hizo, Mwenyekiti wa Chama
cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kinachoandaa bonanza hilo,
Juma Pinto alisema maandalizi kuhusiana
na tamasha hilo linalojulikana kama Media Day Bonanza yamekamilika.
Alisema
wameichukua Extra Bongo inayoongozwa na Ally Choki na Jahazi Modern
inayoongozwa na Mzee Yusuph kutokana na makundi hayo kuwa juu hivi sasa katika
muziki kwa maeneo yao.
“Tunaamini
watakaokuja kwenye tamasha watakuwa na furaha ya aina yake na tumejiandaa vya
kutosha,” alisema Pinto na kueleza kuwa bonanza hilo litafanyika viwanja vya
Sigara Chang’ombe, Dar es Salaam na mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk.
Harrison Mwakyembe.
Pia Pinto alisema
bendi ya Msondo Ngoma Music itapiga kwenye viwanja hivyo kuanzia saa moja usiku
baada ya bendi za Extra Bongo na Jahazi kumaliza kutumbuiza Media Day na kwamba
imetoa ofa kwa wanahabari watakaotaka kubaki kuendelea kupata burudani mpaka
usiku wa manane.
“Msondo wana bonanza lao kila Jumamosi, sasa wamekubali kwamba wanahabari watakaotaka kubaki baada ya bonanza kumalizika jioni wabaki wajiunge na Msondo Ngoma,” alisema Pinto.
Bonanza
hilo la TASWA linadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) likiwa na lengo la
kuwaweka pamoja waandishi wote wa habari bila kujali ni wa siasa, michezo,
uchumi, afya na mambo mengine pamoja na wafanyakazi wa vyombo mbalimbali vya
habari ili kubadilishana mawazo na kufurahi pamoja.
Kwa
upande wake Ofisa Uhusiano wa TBL, Doris Malulu alisema wamejipanga vya kutosha
na kwamba wadau wafike kwa wingi kuhakikisha mambo yanaenda kama yalivyopangwa.
“TBL
ni mdau mkubwa wa wanahabari, tumewaandalia mambo mazuri, naomba msikose,”
alisema Malulu na kuongeza kuwa wanaamini wadau 1,500 kutoka vyombo mbalimbali
vya habari wanaotarajiwa kushiriki bonanza hilo watafurahi vya kutosha siku
hiyo.
Naye Choki
akizungumza kwenye mkutano huo, alisema vijana wake wamejipanga vya kutosha
kushambulia na kuwa dhamira yao ni kuona wana habari wanafurahi vya kutosha na
kuwa mambo waliyowaandalia kila mtu atafurahi kuiona Extra Bongo.
0 maoni:
Post a Comment