KLABU
ya Yanga na Kocha Msaidizi wa timu ya Toto Africans, Athuman Bilali
wamepigwa faini ya sh. 500,000 kila mmoja kutokana na makosa mbalimbali
katika mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inayoendelea nchini.
Adhabu
hizo zimetolewa na Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) iliyokutana Jumapili (Aprili 7 mwaka huu) jijini Dar es
Salaam kupitia ripoti za waamuzi na makamishna kwa michezo namba 108
hadi 171.
Yanga
imepigwa faini hiyo baada ya kupata kadi tano za njano katika mechi
dhidi ya Kagera Sugar iliyochezwa Februari 7 mwaka huu. Vilevile Kagera
Sugar imepigwa faini ya sh. 100,000 kwa kuchelewa kufika kwenye kikao
cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) dhidi ya African Lyon
iliyochezwa mjini Bukoba, Februari 23 mwaka huu.
Naye
Kocha Bilali amepigwa faini hiyo na kufungiwa mechi tatu za ligi hiyo
kwa kumshambulia kwa maneno kocha wa timu pinzani, hali iliyosababisha
mwamuzi amtoe kwenye benchi la wachezaji. Alifanya tukio hilo kwenye
mechi kati ya Toto Africans na Tanzania Prisons iliyochezwa Aprili 3
mwaka huu jijini Mwanza.
African
Lyon na Simba zimepigwa faini ya sh. 500,000 kila moja kwa kushindwa
kuchezesha timu zao za U20 kwenye mechi za utangulizi wakati zilipocheza
na Oljoro JKT na Coastal Union, Machi mwaka huu kwenye viwanja vya Azam
Complex na Uwanja wa Taifa.
Suala
la Meneja wa Coastal Union, Akida Manchai kumshambulia kwa maneno
yasiyo ya kiungwana Makamu Mwenyekiti wake Steven Mnguto baada ya kwenye
mechi kati ya African Lyon na Coastal Union iliyochezwa Machi 30 mwaka
huu Uwanja wa Azam Complex limepelekwa Kamati ya Nidhamu kwa ajili ya
hatua za kinidhamu.
Adhabu zote zimetolewa kwa mujibu wa Kanuni za Ligi Kuu ya Vodacom.
0 maoni:
Post a Comment