Tuesday, April 9, 2013

POLISI KUJIULIZA KWA RUVU SHOOTING VPL

 
Polisi Morogoro inapambana na Ruvu Shooting katika moja kati ya mechi tatu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zitakazochezwa kesho (Aprili 10 mwaka huu). Matokeo ya mechi hiyo yanatarajia kutoa mwanga kama Polisi inaweza kubaki kwenye ligi hiyo msimu ujao.

Timu hiyo itakuwa nyumbani Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro katika mechi hiyo itakayochezeshwa na Ibrahim Kidiwa kutoka Tanga akisaidiwa na Godfrey Kihwili na Ephrony Ndissa wa Arusha.

Polisi Morogoro inayonolewa na Adolf Rishard inakamata nafasi ya mwisho ikiwa na pointi 18 tu na imebakiza mechi tatu dhidi ya Simba, Kagera Sugar na Coastal Union.

Mechi nyingine za kesho ni kati ya Tanzania Prisons iliyo nafasi ya 12 ikiwa na pointi 20 dhidi ya Mgambo Shooting. Mwamuzi Hashim Abdallah wa Dar es Salaam ndiye atakayechezesha mechi hiyo kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya. Mgambo ina pointi 24 na iko katika nafasi ya tisa.

Mwamuzi Said Ndege wa Dar es Salaam atachezesha mechi kati ya wenyeji Mtibwa Sugar na Toto Africans itakayofanyika Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro. Toto Africans ya Kocha John Tegete ina pointi 21 ikiwa nafasi ya 11 wakati Mtibwa Sugar iko nafasi ya tano na pointi zake 32.

Ligi hiyo itaendelea keshokutwa (Aprili 11 mwaka huu) kwa mechi moja kati ya Azam na African Lyon itakayofanyika Uwanja wa Azam Complex.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU