Kocha wa
Timu ya Taifa, Kim Poulsen na Nahodha Juma Kaseja wakati wa mkutano na
waandishi wa habari katika hoteli ya Pullman ilikoyo Marrakech.
Huku Timu ya
Taifa Taifa Stars ikikabiliwa na mechi muhimu kesho (Jumamosi) dhidi ya Morocco
kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia, Kocha Kim Poulsen amesema
amejiandaa kucheza mpira wa kasi na wenye pasi za uhakika ili kuivuruga beki ya
Morocco.
Kocha huyo
ameyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari na kusisitiza kuwa ni
muhimu kuhakikisha Morocco hawaupati mpira kwa urahisi.
“Wachezaji
wako katika hali nzuri kabisa na wana ari ya kushinda mechi hii…tuna nguvu na
tunajua namna ya kuwapiga Morocco,” alisema kocha huyo.
Alisema
suala si mchezaji gani anaanza au washambulizi ni wangapi, bali ni kazi
itakayofanyika uwanjani na ubora wa wachezaji wa Taifa Stars, inayofurahia
udhamnini mnono wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager.
Alisema
Morocco ni timu kubwa na ina wachezaji wengi wa kulipwa lakini inafungika na
Taifa Stars itaweka nguvu kuanzia mwanzo wa mechi.
“Unapocheza
mechi kama hii inabidi uweke nguvu dakika za kwanza za mechi ili umpe mpinzani
wakati mgumu kwa hivyo dakika za mwanzo zitakuwa muhimu sana katika mechi hii,”
alisema.
Poulsena
alisema baadhi ya watu nchini Morocco bado wanaamini kuwa ushindi wa mechi ya
awali Jijini Dar es Salaam wa 3-1 dhidi ya Morocco ulikuwa wa kibahati tu. “Tunataka
kuwadhihirishia kuwa tunaweza na Taifa Stars sio timu ndogo kama wanayodhani.”
Alisema
mazingira ya kambi ni mazuri kabisa na wachezaji wote wako katika hali nzuri na
tayari kwa mchezo huu.
“Katika hali
ya kawaida ungetegemea hujuma nyingi ikiwemo hoteli mbovu, viwanja vibovu vya
mazoezi na kadhalika lakini hapa ni tofauti kabisa…kwani mazingira ni mazuri,”
alisema Poulsen.
Taifa Stars
imeweka kambi katika Hoteli ya Pullman iliyoko nje kidogo ya Mji wa Marrakech.
Naye nahodha
wa Taifa Stars, Juma Kaseja alisema wamefanya mazoezi ya kutosha hasa
ikizingatiwa kambi ilianzia Addis Ababa, Ethiopia ambako walicheza mechi ya
kirafiki na Sudan na kutoa sare ya 0-0 kabla ya kuelekea Marrakech.
“Morocco ni
timu kubwa, tunapaswa kuiheshimu lakini sio kuiogopa…tutapambana ili timu ipate
matokeo,” alisema Kaseja.
Naye Meneja
wa Bia ya Kilimanajro Premium Lager, George Kavishe, akizungumza kutoka Dar es
Salaam alisema wao kama wadhamini wa Taifa Stars wana imani kubwa sana na Stars
na wanaitaka iwape Watanzania raha kwa mara nyingine kwa kushinda mechi hiyo.
“Tumewaona
wakifanya vizuri nyumbani kwa kushinda mechi tano mfululizo na sasa ni muda wa
kupata ushindi nje,” alisema.
Stars iko
katika kundi C pamoja na Ivory Coast, Morocco na Gambia. Kundi hilo linaongozwa
na Ivory Coast yenye pointi 7, Tanzania 6, Morocco 2 na Gambia 1.
Mechi ya
kesho itapigwa katika Uwanja wa Marrakech saa tatu usiku kwa saa za Morocco
ambayo itakuwa saa tano kamili Tanzania.
Baada ya
Morocco Stars itacheza na Ivory Coast nyumbani Jumapili ijayo na mechi ya
mwisho itakuwa dhidi ya Gambia Septemba mwaka huu.
0 maoni:
Post a Comment