Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za
kifo cha kocha wa zamani wa Taifa Stars, Bert Trautmann (89)
kilichotokea jana (Julai 19 mwaka huu) nchini Hispania.
Kabla
ya kuwa kocha, Trautmann aliyezaliwa 1923 mjini Bremen, Ujerumani
alikuwa kipa wa timu ya Manchester City ya Uingereza ambapo anakumbukwa
kwa kucheza mechi ya fainali ya Kombe la FA dhidi ya Birmingham City
akiwa amevunjika shingo.
Manchester
City ilishinda fainali hiyo iliyochezwa mwaka 1956 mabao 3-1. Trautmann
ambaye aligongana na mshambuliaji wa Birmingham, Peter Murphy zikiwa
zimesalia dakika 17 mechi hiyo kumalizika aligundua kuwa amevunjika
shingo siku tatu baadaye.
Mbali
ya kuwa kocha wa Taifa Stars mwanzoni mwa miaka ya 60, Trautmann pia
alikuwa mkufunzi wa makocha ambapo hapa nchini aliendesha kozi
mbalimbali zilizotoa makocha waliokuja kutamba baadaye.
TFF
itamkumbuka Trautmann kwa mchango wake aliotoa katika maendeleo ya
mpira wa miguu nchini ikiwemo wazo lake la kuanzishwa kwa Ligi Kuu
(Daraja la Kwanza) ambalo alilitekeleza katikati ya miaka ya 60.
Msiba
huo ni pigo kwa familia ya Trautmann, TFF na familia ya mpira wa miguu
kwa ujumla nchini kutokana na mchango alioutoa kwa Tanzania hasa wakati
akiwa kocha na mkufunzi wa makocha.
TFF
inatoa pole kwa familia ya marehemu Trautmann, Chama cha Mpira wa Miguu
cha Ujerumani (DFB), Chama cha Mpira wa Miguu cha Uingereza (FA) na
kuwataka kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki cha msiba huo mzito.
Mungu aiweke roho ya marehemu Bert Trautmann mahali pema peponi. Amina
0 maoni:
Post a Comment