Friday, July 12, 2013

TAIFA STARS SASA MMEIVA KUPAMBANA- TENGA

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema kikosi cha Taifa Stars sasa kina uwezo wa kushindana katika mashindano yoyote, kwani tayari kimeiva.

Akizungumza na wachezaji wa timu hiyo kambini kwao hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam, Rais Tenga aliwaambia kuwa kiwango walichoonesha kwenye mechi zilizopita za mchujo za Kombe la Dunia dhidi ya Morocco na Ivory Coast kimethibitisha hilo.

“Kiwango mlichoonyesha katika mechi hizo kila Mtanzania anayewafuatilia amekiona, hivyo hatuna shaka kuwa mtatuwakilisha vizuri kwenye mechi ya kesho dhidi ya Uganda,” amesema Rais Tenga na kuwataka kupigana kwa ajili ya Tanzania.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager kesho (Julai 13 mwaka huu) saa 9 kamili alasiri Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam itacheza na Uganda (The Cranes) katika mechi ya kwanza ya raundi ya mwisho kuwania tiketi ya kucheza Fainali za CHAN zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.

Rais Tenga amesema TFF, mdhamini Kilimanjaro Premium Lager, Kamati ya Ushindi na Watanzania kwa ujumla wanawaunga mkono kwani wamekuwa wakiboresha kiwango chao kila wanavyozidi kucheza mechi tangu wake chini ya Kocha Kim Poulsen, Mei mwaka jana.

Wakati huo huo, Rais Tenga ameahidi kumpatia tiketi ya kwenda Uganda kwenye mechi ya marudiano mshabiki Wiseman Mwakyusa Luvanda anayetembea kwa miguu kutoka Mbeya kuja Dar es Salaam kushuhudia mechi ya kesho.

“Kama ni kweli anakuja kwa kutembea, huyu ameonyesha kiwango kikubwa cha uzalendo kwa timu ya Taifa, nitampatia tiketi ya kwenda Kampala kuishangilia Taifa Stars kwenye mechi ya marudiano,” amesema Rais Tenga.

…POULSEN, MICHO WATABIRI MECHI KALI
Makocha wa timu hizo Kim Poulsen wa Taifa Stars na Sredojvic Micho wa The Cranes wamesema mechi ya kesho itakuwa ngumu kwa vile kila mmoja amejiandaa kuhakikisha anafanya vizuri.

Wakizungumza na Waandishi wa Habari leo, makocha wote waliezea ubora wa wapinzani wao, lakini wakasisitiza kuwa wanaingia uwanjani kuhakikisha wanashinda ili kujiweka katika mazingira mazuri kwa ajili ya mechi ya marudiano itakayochezwa Kampala wiki mbili zijazo.

Kim alisema Uganda ndiyo inayoongoza kwa ubora wa viwango vya FIFA katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, hivyo ni changamoto kwao ingawa wachezaji wake tayari wamejipanga vizuri kwa ajili ya mechi hiyo.

Naye Micho aliyefuatana na nahodha wake Hassan Wasswa alisema Taifa Stars imekuwa ikifanya vizuri tangu iwe chini ya Kim, na itakuwa na wachezaji tisa wa kikosi cha kwanza kinachocheza mechi za mchujo za Kombe la Dunia wakati kwa upande wake atakuwa na wachezaji wawili tu.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU