SHULE
Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam (UDSM) kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo
Tanzania (TASWA) wataendesha mafunzo ya siku tano kwa waandishi wa habari za
michezo nchini.
Akizungumza
kwenye mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Makamu Mkuu wa SJMC,
Dk. Michael Andindilile alisema mafunzo hayo yatafanyika Agosti mwaka huu na
yataendeshwa na wahadhiri kutoka chuoni hapo, waandishi wa siku nyingi na
wataalamu wa michezo mbalimbali.
“Tunao
wahadhiri waliobobea katika tasnia ya habari, lakini pia wapo waandishi wa
habari wakongwe ambao ni waalimu kitaaluma, pia tutachukua wataalamu wa michezo
mbalimbali kuja kufundisha kwa siku hizo tano,” alisema Dk. Andindilile.
Makamu
Mkuu huyo wa SJMC, aliupongeza uongozi wa TASWA kwa wazo lao la kushirikiana na
SJMC na kuongeza kuwa mafunzo hayo yatachukua siku tano na yatafanyika Dar es
Salaam yakihusisha washiriki 45 kutoka vyombo mbalimbali vya habari katika
tarehe itakayotangazwa.
Alisema
wataalamu wa michezo mbalimbali kama vile soka, riadha, netiboli, gofu, kikapu,
wavu na mikono watapata fursa ya kutoa mada kuhusiana na michezo yao na kwamba
TASWA na SJMC wanashirikiana katika kuomba wadhamini wasaidie mafunzo hayo.
“Hii
ni awamu ya kwanza kwa waandishi wachanga na baadhi ya wa kada ya kati, baada
ya hapo tutaendesha mafunzo ya namna hii kwa waandishi wa siku nyingi wa habari
za michezo na wahariri wa habari za michezo, tunaamini baada ya hapo kutakuwa
na mabadiliko upande wa uandishi wa habari za michezo,” alisema.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto aliishukuru SJMC kwa kukubali
kushirikiana na TASWA na kwamba siku zote chama chake kimekuwa kikipigania
kuandaa mafunzo kwa wanahabari wa michezo kama sehemu mojawapo ya kukuza
weledi.
“Fursa
hii ni moja ya jitihada za TASWA kuhakikisha waandishi wa habari za michezo
wanapata nafasi ya kujifunza zaidi kuhusu namna bora ya kuripoti habari za michezo
kwa ujumla wake, hivyo nafasi hii si tu itasaidia wanachama wa TASWA bali pia
na vyombo vya habari na washiriki hawatalipia chochote.
“Tunaamini
waandishi wanapoboresha uandishi wao inachangia kwa kiasi kikubwa kukuza
heshima ya vombo vya habari, hivyo tunaomba wadau mbalimbali washirikiane nasi
kudhamini mafunzo haya,” alisema Pinto na kuongeza kuwa kwa kushirikiana na
SJMC wanaamini siku za usoni wanaweza kuandaaa mafunzo ya muda mrefu.
0 maoni:
Post a Comment