Mamlaka
za Mkoa wa Mwanza zimesema zitatimiza ahadi yao ya kuchangia dola
118,000 za Marekani (zaidi ya sh. milioni 190) ili kukamilisha mradi wa
kuweka nyasi bandia kwenye Uwanja wa Nyamagana, jijini Mwanza kabla ya
Oktoba 15 mwaka huu.
Mkuu
wa Mkoa (RC) wa Mwanza, Mhandisi Evarist Ndikilo pamoja na Mstahiki
Meya wa Jiji la Mwanza, Stanslaus Mabula wametoa ahadi hiyo wakati wa
kikao kati yao na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),
Leodegar Tenga kilichofanyika leo (Septemba 25 mwaka huu) kwenye ofisi
za TFF.
Wakuu hao wa Mwanza katika kikao hicho pia walifuatana na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Hida Hassan.
TFF
ilipeleka mradi wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) wa
Goal Project IV wa nyasi bandia wa dola 500,000 za Marekani katika
Uwanja wa Nyamagana.
Mradi
huo ulipelekwa huko baada ya Mkoa wa Mwanza kuahidi kuchangia dola
118,000 ili kukamilisha thamani ya mradi mzima ambayo ni dola 618,000 za
Marekani. Wamiliki wa uwanja huo ni Jiji la Mwanza.
Goal
Project I ilitumika kwa ajili ya ujenzi wa hosteli ya TFF (technical
centre), Goal Project II nyasi bandia Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume
wakati Goal Project III iliweka nyasi bandia katika Uwanja wa Gombani
ulioko Pemba, Zanzibar.
Captions:
Rais wa TFF, Leodegar Tenga (wa pili kushoto) akiwa na ujumbe wa Mkoa
wa Mwanza ulioongozwa na Mkuu wa Mkoa, Mhandisi Evarist Ndikilo
ulipomtembelea katika ofisi za TFF jana. Wa tatu kutoka kushoto ni
Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, Stanslaus Mabula akifuatiwa na
Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Hida Hassan.
0 maoni:
Post a Comment