Friday, October 25, 2013

HAMAD YAHYA JUMA NDIYE MWENYEKITI WA BODI YA LIGI

Hamad Yahya Juma wa Mtibwa Sugar ndiye Mwenyekiti wa kwanza wa Bodi ya Ligi Tanzania (Tanzania Professional League- TPL Board) baada ya kushinda katika uchaguzi uliofanyika leo mchana (Oktoba 25 mwaka huu) kwenye ukumbi wa mikutano uliopo Golden Jubilee Tower, Dar es Salaam.


Juma ambaye hakuwa na mpinzani alipata kura zote kumi za ndiyo zilizopigwa na klabu za Ligi Kuu zilizohudhuria mkutano huo. Klabu ambazo hazikuhudhuria uchaguzi huo ni JKT Ruvu, Mgambo Shooting, Coastal Union na Rhino Rangers.


Naye Said Muhammad Said Abeid ambaye pia hakuwa na mpinzani amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti kwa kupata kura zote za ndiyo.


Kwa upande wa wajumbe wawili wa Kamati ya Uendeshaji, wote Kazimoto Miraji Muzo wa Pamba na Khatib Omari Mwindadi wa Mwadui wameshinda kwa kura zilizopigwa na klabu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL).


Muzo alipata kura 15 za ndiyo wakati mbili zikimkataa, huku Mwindadi akipata kura 16 na moja ilimkataa. Klabu za FDL ambazo hazikuhudhuria uchaguzi huo ni Transit Camp, Burkina Faso, Polisi Mara, Stand United, Toto Africans, Polisi Tabora na Kanembwa JKT.

MSUMBIJI U 20 WATUA KUIKABILI THE TANZANITE.

Timu ya Taifa ya wanawake kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 imewasili nchini leo (Ijumaa, Oktoba 25 mwaka huu) saa 8.45 mchana tayari kwa mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza ya Kombe la Dunia dhidi ya Tanzania itakayofanyika kesho (Jumamosi).


Msumbiji imetua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa ndege ya LAM ikiwa na msafara wa watu 25 unaohusisha wachezaji, benchi la ufundi na viongozi, na kwenda moja kwa moja kwenye hoteli ya Sapphire.


Msumbiji ilitarajia jioni hii (saa 11) kufanya mazoezi yake ya kwanza na ya mwisho ikiwa nchini kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Kwa upande wa The Tanzanite, Kocha Rogasian Kaijage amesema wamejiandaa vizuri na wako tayari kwa ajili ya mechi hiyo ambayo matokeo yake ndiyo yatakayoamua mikakati yake kwa ajili ya mechi ya marudiano itakuwaje.


Viingilio kwa mechi hiyo ni sh. 1,000 kwa viti vya rangi ya kijani, bluu na rangi ya chungwa. Viingilio vingine ni sh. 2,000 kwa VIP C, sh. 5,000 kwa VIP B wakati VIP A itakuwa sh. 10,000. Tiketi zitauzwa katika magari maalumu uwanjani.


Naye Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi uwanjani ili kuiunga mkono The Tanzanite ili iweze kufanya vizuri kwenye mechi hiyo.

TUNAFURAHI KUSIKIA AJENDA- TENGA.

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) anayemaliza muda wake, Leodegar Tenga amesema amefurahishwa na jinsi kampeni za uchaguzi zinazokwenda kutoka na ukweli kuwa wagombea wamekuwa wakielezea kile wanachotaka kuufanyia mpira wa miguu.


Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za TFF leo mchana, Rais Tenga ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) amesema Watanzania wanataka kusikia ajenda za wagombea.


“Ombi langu ni kwamba kampeni zimeanza vizuri, watu wanazungumza hoja zaidi. Ni jukumu la wajumbe kupima na kufanya uamuzi. Kwangu mimi nimejitayarisha kumkabidhi Katiba, Rais mpya wa TFF,” amesema.


Tenga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) amesema kazi kubwa iliyofanywa na uongozi wake ni kujenga taasisi (TFF) pamoja na kuweka mifumo (structure) inayoainisha majukumu ya kila mmoja.


“Ajenda yetu wakati tunaingia madarakani mwaka 2005 ilikuwa ni kujenga taasisi. Tayari taasisi ipo, sasa mtazamo uwe kuushughulia mpira wa miguu wenyewe,” amesema.


Mkutano Mkuu wa TFF unafanyika kesho kwenye ukumbi wa mikutano wa NSSF Waterfront, na tayari wajumbe wa mkutano huo ambao pia utakuwa na ajenda ya uchaguzi siku inayofuata wameshawasili jijini Dar es Salaam.


Wawakilishi kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Ashford Mamelodi ambaye ni Ofisa Maendeleo wa kanda hii, Magdi Shams El Din ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF na Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) ni miongoni mwa wageni watakaohudhuria mkutano huo.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU