Thursday, October 3, 2013

TAMASHA LA UTAMADUNI HUKO HANDENI TANGA LAPAMBA MOTO



WADAU wa mambo ya utamaduni na michezo wameombwa kujitokeza kwa wingi kufanikisha kufanyika kwa Tamasha la Utamaduni lililopangwa kufanyika Desemba 14 mwaka huu wilayani Handeni, mkoani Tanga.
Mratibu wa Tamasha la Utamaduni wilayani Handeni, mkoani Tanga, Kambi Mbwana, pichani.

Hayo yamesemwa na mratibu wa tamasha hilo, Kambi Mbwana, alipozungumza na mwandishi wa mtandao huu mapema leo jijini Dar es Salaam, ikiwa ni siku chache baada ya kutangaza mipango ya kuandaa tamasha hilo la aina yake na lenye mguso wa kuwakutanisha wadau wote kwa pamoja kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Akizungumzia maandalizi ya tamasha hilo, Mbwana alisema endapo wadau wote, wakiwamo wafanyabiashara na wamiliki wa kampuni, taasisi za serikali watashirikiana katika hilo, mambo yatakuwa mazuri.

Alisema hali hiyo inamfanya aone haja ya kuwataka watu hao washirikiane kwa pamoja kwa ajili ya kuhakikisha kuwa tamasha la utamaduni na michezo Handeni linafanyika kwa mafanikio na kuweka historia mpya.



Kwa mujibu wa Mbwana, kufanyika kwa tamasha hilo kutakuwa ni sehemu nzuri ya kuwakutanisha wadau, wananchi wa Handeni na Tanzania kwa ujumla kwa ajili ya kujadiliana changamoto zinazowakabili kwa maendeleo yao.

Tamasha hilo la Utamaduni linaandaliwa chini ya Raha Company and Entertainment huku likifanyika kwa mara ya kwanza katika wilaya hiyo inayoongozwa na Mkuu wake wa Wilaya Muhingo Rweyemamu, wakati mbunge ni Dk Abdallah Omari Kigoda ambaye pia ni Waziri wa Viwanda na Biashara.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU