Sunday, November 10, 2013

TIDO MHANDO AJITOKEZA UHURU MARATHON

USAJILI wa mbio za Uhuru Marathon, ulioanza kwa kishindo wiki iliyopita pale Spika wa Bunge, Anne Makinda alipowaongoza wabunge kufanya hivyo, unazidi kushika kasi huku Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications, Tido Mhando naye akiahidi kujisajili leo ili aweze kushiriki.
 
Kampuni hiyo ni wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na gazeti la michezo la Mwanaspoti.
 
Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu wa Kamati ya Uhuru Marathon, Innocent Melleck alisema, Tido anatarajiwa kujisajili kushiriki mbio hizo, baada ya kuvutiwa na lengo lake ambalo ni kuimarisha amani, umoja na mshikamano.
 
Melleck hakutaka kufafanua Tido anataka kushiriki mbio za kilomita ngapi, ingawa alisema zitatolewa kwa Sh 100,000 kwa wale watakaokimbia mbio za kilomita tatu, Sh 2,000 mbio za kilomita tano, Sh 6,000 kwa atakayeshiriki moja kati ya mbio za kilomita 21 au 42.
 
“Hizi mbio ni muhimu zaidi kwa ajili ya Taifa letu, hivyo ni vyema kwa Watanzania wote wakashiriki ili kuipigania amani iliyopo nchini mwetu na ndiyo maana hata Rais Jakaya Kikwete, pia atashiriki.
 
“Kesho (leo) Tido anatarajiwa pia kujisajili kwa ajili ya kushiriki mbio hizo, lengo kubwa ikiwa pia kushawishi Watanzania wengine waweze kushiriki,” alisema.
 
Mratibu huyo alisema mbio za kilomita 3 zitakuwa maalumu kwa ajili ya viongozi wa kada mbalimbali, wakiwemo pia wale wa dini na zile za kilomita 5 pia zitakuwa za kuchangia kwa ajili ya watu wa mahitaji maalumu.
 
“Hapa tunachotaka kufanya katika mbio za kilomita 3 mbali na Rais Kikwete, pia tunawaomba viongozi maarufu wa dini mbalimbali pamoja na viongozi wetu kada nyingine kushiriki, kwa kudumisha amani na upendo.
 
“Pia tutahakikisha kama mbio za kilomita 5, zinakuwa kwa ajili ya kuchangia watu wenye mahitaji maalumu na tayari tuna uhakika mkubwa wa wanariadha maarufu zaidi duniani kushiriki,” alisema.
 
Mbio hizo zinatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam hapo Desemba 8, mwaka huu na zitaanzia na kuishia katika Viwanja vya Leaders vilivyopo Kinondoni.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU