Huku Spika
wa Bunge, Anne Makinda akiongoza wabunge zaidi ya 100 kujisajili kwa ajili ya
kushiriki mbio ndefu za Uhuru, maarufu kama Uhuru Marathon zinazotarajiwa
kufanyika Dar es Salaam Desemba 8, mwaka huu tayari kampuni na taasisi kadhaa
zimejitokeza kudhamini mbio hizo.
Wakati
akijiandikisha kwa ajili ya kushiriki mbio hizo zenye lengo la kuwasisitiza
Watanzania kuhusu umuhimu wa kutunza amani, umoja na mshikamano miongoni mwetu,
Makinda alisema ni wakati wa kila Mtanzania kushiriki kwa njia moja au nyingine
kupigania vitu hivyo.
“Naomba na
nawasisitiza wabunge na viongozi mbalimbali kushiriki mbio hizi, kwani zina
lengo zuri na lenye kuleta tija kwa Taifa letu.
“Mbio hizi
zinatukumbusha ni lazima tuwe na amani, umoja na mshikamano, iwe ndani ya Bunge
au hata nje, hivyo nategemea kuona wabunge wengi zaidi wakishiriki,” alisema.
Katibu wa
Kamati ya Uhuru Marathon, Innocent Melleck alisema, kauli ya Spika Makinda ni
kama kichocheo zaidi kwani kwa sasa kumejitokeza idadi kubwa ya kampuni,
taasisi na hata watu binafsi wanaotaka kudhamini mbio hizo.
Melleck
alisema, wanatarajia kutangaza wadhamini wa awali siku yoyote kuanzia kesho na
kutaka wengine kuendelea kujitokeza kwa ajili ya mbio hizo.
Aidha
alifafanua kuwa, fomu hizo zinatolewa kwa Sh 100,000 kwa wale watakaokimbia
mbio za kilomita tatu, Sh 2,000 mbio za kilomita tano, Sh 6,000 kwa
atakayeshiriki moja kati ya mbio za kilomita 21 au 42.
“Hizi mbio
ni muhimu zaidi kwa ajili ya Taifa letu, hivyo ni vyema kwa Watanzania wote
wakashiriki ili kuipigania amani iliyopo nchini mwetu na tumefurahishwa na mno
na watu waliojitokeza kushiriki mpaka sasa.
“Kwetu sisi
tunataka kuungana na Rais Jakaya Kikwete katika kuhakikisha tunakuwa sehemu ya
kuleta umoja, amani na mshikamano ndani ya Tanzania na ndilo lengu la mbio
hizi.”
Mratibu huyo
anasema mbio za kilomita 3 zitakuwa maalumu kwa ajili ya viongozi wa kada
mbalimbali, wakiwemo pia wale wa dini na zile za kilomita 5 pia zitakuwa za
kuchangia kwa ajili ya watu wa mahitaji maalumu.
Uhuru Marathon ni mbio zinazosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki, hasa
kutoka na lengo lake kubwa ambalo ni kutukumbusha kuhusu kulinda amani na
kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwetu.
0 maoni:
Post a Comment