Andy Cole akionyesha umahiri wake katika
kulisakata kabumbu alipokuwa akitoa somo kwa wanafunzi wa Shule ya
Sekondari ya Makongo ya jijini Dar es salaam mara ya mwisho
alipotembelea Tanzania.
MCHEZAJI wa zamani wa klabu ya Manchester United Andy Cole anatarajia kutua jijini Dar es Salaam Ijumaa hii, imethibishwa.
Ziara ya Cole nchini
inalenga kuwapatia uzoefu washindi wa tiketi za promosheni ya Airtel ya
'Mimi ni Bingwa' ambao watasafiri kwenda kuangalia mechi za klabu ya
Manchester United moja kwa moja (live) katika uwanja wa Old Trafford
pamoja na kukabidhi vifaa vya mazoezi kwa wachezaji wa timu ya taifa ya
Tanzania ya chini ya umri wa miaka 17.
Hii ni ziara ya pili
Tanzania kwa mchezaji Cole baada ya kutembelea Tanzania mwaka 2011
alipozindua mpango wa kutafuta vipaji wa Airtel Rising Star.
Akizungumza na
waandishi wa habari juu ya ziara hiyo, Meneja Uhusiano wa kampuni ya
mawasiliano ya Airtel Tanzania, Bw Jackson Mmbando alisema kuwa mchezaji
huyo mkubwa wa zamani wa Man U atakuwa na wakati wa kuzungumza na
kushiriki mazoezi na wachezaji wa timu ya Tanzania chini ya miaka 17,
timu ambayo wengi wao ni matunda ya mpango wa kuvumbua vipaji wa Airtel
Rising Star.
"Andy Cole ataongea na
nyota hao wanaochipukia, na kuwashawishi kuongeza jitihada zaidi katika
michezo pamoja na kuwapatia mbinu za jinsi gani ya kufikia mafanikio
katika fani yao ya michezo.
"Mbali na kuwaonyesha
wachezaji hao njia ya mafanikio, mchezaji huyo mkubwa wa zamani wa
Manchester United pia atakabidhi vifaa vya mazoezi kwa timu hiyo,"
alisema Mmbando.
Alisema kuwa Cole pia
atahudhuria droo ya moja kwa moja (live) ya kuwatafuta na kuwatangaza
washindi wa tiketi tatu za kwenda Old Trafford, kabla ya kuungana na
washabiki wa Man U kuangalia mechi moja kwa moja (live) itakayoonyeshwa
Coco beach kati ya Manchester United na Aston Villa itakayochezwa
jumapili.
Rashid Jacob Kagomola
na Dickson Lyatuu ni washindi wa kwanza wawili wa promosheni ya Mimi ni
Bingwa waliojishindia tiketi za kwenda Old Trafford, ambapo zawadi zaidi
ya shilingi milioni 40 tayari imetolewa kwa ajili ya washindi wa kila
siku na kila wiki.
Mmbando alisema kuwa
bado kuna zawadi nyingi zaidi kushindaniwa katika promosheni, na
kuongeza kuwa ili mteja kushiriki anatakiwa kutuma ujumbe mfupi (SMS) wa
neno "BINGWA" kwenda namba 15656.
Aidha, alisema Airtel
imeweka vituo mbali mbali ambavyo washabiki wa Man U wataweza kuangalia
mechi za Manchester United moja kwa moja (live) kupitia luninga kubwa,
na kutaja vituo hivyo kuwa ni Mbeya - Shaba Pub, Mwanza - Shooters Pub,
Dodoma - Four ways, Dar es Salaam - Coco Beach, Morogoro - Nyumbani
Lounge na Arusha - Empire Sports bar.
Mwaka 2011 kampuni ya
mawasiliano ya Airtel Tanzania ilizindua mpango wa kuvumbua vipaji
katika soka kwa ushirikiano na klabu ya Manchester United, uliolenga
kuvumbua vipaji na kuviendeleza katika mpira wa miguu Tanzania.
Cole amekuwa na
dhamira ya kuonyesha uzoefu wake kwa wachezaji nyota wanaochipukia ikiwa
ni kama njia ya kuunga mkono maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu
duniani.
0 maoni:
Post a Comment