Saturday, February 22, 2014

RAIS MALINZI AAHIDIWA USHIRIKIANO CAF

 Rais wa TFF, Jamal Malinzi akiwa na Rais wa CAF, Issa Hayatou
 Rais wa TFF, Jamal Malinzi akiwa na Rais wa CAF, Issa Hayatou na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF, Leodegar Tenga makao makuu ya CAF jijini Cairo, Misri.


Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemwahidi ushirikiano Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi.

Ahadi hiyo imetolewa leo (Februari 21 mwaka huu) makao makuu ya CAF jijini Cairo na Rais wa shirikisho hilo Issa Hayatou alipokutana na Rais Malinzi aliyekwenda kujitambulisha huko.

Utambulisho wa Rais Malinzi kwa Rais Hayatou uliongozwa na mtangulizi wake Leodegar Tenga ambaye aliiongoza TFF kwa vipindi viwili kuanzia 2004 hadi 2013.

Tenga ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF na Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), alimweleza Rais Hayatou kuwa uchaguzi wa TFF ulikuwa mzuri.

Aliongeza kuwa alimkabidhi kijiti Rais Malinzi kwa maridhiano na ana imani na uongozi wake.
Rais Hayatou alimpokea Rais Malinzi na kuahidi kuendelea kuipa Tanzania ushirikiano hasa katika maeneo ya utawala, ufundi na kuboresha miundombinu ya kuendeleza mpira wa miguu.

Kwa upande wake, Rais Malinzi alisema TFF itaendelea kutoa ushirikiano wa dhati kwa CAF ili kuhakikisha kiwango cha mpira wa miguu nchini Tanzania kinakuwa.

Baadaye mchana, Rais Malinzi alipata chakula cha mchana pamoja na wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji ya CAF.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU