Hatua ya robo fainali ya Kili Taifa Cup inaanza Mei 22 mwaka huu Uwanja wa
Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid jijini Arusha. Robo fainali zitachezwa mechi
mbili kwa siku. Ya kwanza saa 8.00 mchana na ya pili saa 10.00 jioni.
Mei 22 mechi ya kwanza ni Singida (Kindai Shooting Stars) na Ilala. Mechi ya
pili ni Mwanza (Mwanza Heroes) na Arusha (Mount Meru Warriors). Mei 23 mechi ya
kwanza ni Mbeya na Ruvuma (Ruvuma Warriors) wakati ya pili ni timu ya Taifa
chini ya umri wa miaka 23 (U23) na Kagera (Lweru Eagles).
Nusu fainali ya kwanza itakayohusisha washindi wa robo fainali za Mei 22
itachezwa Mei 24. Ya pili itachezwa Mei 25 wakati Mei 26 itakuwa mapumziko.
Mechi ya mshindi wa tatu itakuwa Mei 27 na fainali itachezwa Mei 28.
Waamuzi watakaochezesha hatua hiyo ambao wote wana beji za Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ni Israel Mujuni, Judith Gamba na Oden Mbaga.
Waamuzi wasaidizi ni Samwel Mpenzu, Hamis Chan’gwalu, Saada Tibabimale, Zahra
Hussein, John Kanyenye na Erasmus Jesse.
Makamishna wa mechi ni Hakim Byemba na Mrisho Bukuku wakati mtathmini wa marefa
(referee assessor) ni Charles Mchau. Msimamizi wa fainali hizo ni Khalifa Mgonja
ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF).
MALALAMIKO KILI ATAIFA CUP
Kamati ya Mashindano ya TFF iliyokutana leo (Mei 15 mwaka huu) ilipitia taarifa
za michuano hiyo hatua ya makundi ikiwemo malalamiko ya timu za Mara na Dodoma
ambazo zililalamikia usajili wa mchezaji mmoja katika timu za Kigoma na Kagera.
Kamati haikusikiliza malalamiko hayo kwa vile yaliwasilishwa nje ya muda wa
pingamizi.
LIGI YA TAIFA
Ligi ya Taifa inayoshirikisha mabingwa wa mikoa itaanza Juni 11 mwaka huu katika
vituo vya Sumbawanga, Kigoma, Singida na Kibaha. Washindi watatu wa kwanza wa
kila kituo watashiriki hatua ya fainali itakayofanyika katika kituo
kitakachotangazwa baadaye.
Kituo hicho cha fainali kitakuwa na makundi matatu ya timu nne nne. Mshindi wa
kila kundi na washindwa bora (best losers) wawili, hivyo kufanya jumla ya timu
tano ndizo zitakazopanda kucheza Ligi Daraja la Kwanza.
Kituo cha Sumbawanga kitakuwa na timu za Small Kids (Rukwa), Ilonga FC (Mbeya),
Mlale JKT (Ruvuma), Central Police (Dar 3), Tumbaku SC (Morogoro) na mabingwa wa
Iringa. Kituo cha Kigoma kitakuwa na timu za Shinyanga United (Shinyanga), Geita
Veterans (Mwanza), Polisi SC (Mara), Kasulu United (Kigoma), Rumanyika FC
(Kagera) na mabingwa wa Tabora.
Singida itakuwa na timu za Polisi SC (Arusha), Babati Mashujaa SC (Manyara),
Lang’ata Bora FC (Kilimanjaro), Samaria FC (Singida) na Majengo FC (Dodoma).
Kituo cha Kibaha ni Cosmopolitan (Dar 1), Mgambo Shooting (Tanga), Mailimoja
United (Pwani), Sifapolitan (Dar 2), Liwale Stars (Lindi) na mabingwa wa Mtwara.
Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana
leo (Mei 15 mwaka huu) imesisita kuwa iwapo mikoa ya Tabora, Iringa na Mtwara
itakuwa haijawasilisha majina ya mabingwa wao katika muda uliopangwa ligi hiyo
itaendelea bila timu zao kuwemo.
Mwisho wa timu kuthibitisha kushiriki na kulipa ada ya ushiriki ya sh. 70,000 ni
Mei 20 mwaka huu. Mei 28 mwaka huu ndiyo siku ya mwisho ya kurudisha fomu za
usajili.
Boniface Wambura
Ofisa Habari TFF
0 maoni:
Post a Comment