Monday, May 16, 2011

SIMBA v WYDAD CASABLANCA


Mechi ya kutafuta nafasi ya kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika
baada ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kuondolewa kwa
kuchezesha mchezaji asiyestahili imepangwa kufanyika kati ya Mei 27, 28 na 29
mwaka huu kwenye uwanja huru (neutral ground).
 
Simba ya Tanzania na Wydad de Casablanca ya Morocco ndizo zitakazopambana katika
mechi hiyo ya mkondo mmoja. Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF)
linatarajia kutaja katika muda mfupi ujao nchi ambapo mechi hiyo itachezwa.
 
Timu itakayoshinda itaingia katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, ikiwa
kundi B pamoja na Al Ahly ya Misri, Esperence (Tunisia) na Moloudia Club d’Alger
ya Algeria. Timu itakayoshindwa itaingia katika hatua ya 16 bora ya michuano ya
Kombe la Shirikisho ambapo itacheza mechi ya kwanza nyumbani na Daring Club
Motema Pembe ya DRC kati ya Juni 10, 11 na 12 mwaka huu.


MAPATO STARS v BAFANA BAFANA
 
Pambano la kirafiki kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Afrika Kusini (Bafana
Bafana) lililochezwa Mei 14 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza
sh. 75,888,000 kutokana na watazamaji 10,554 walionunua tiketi.Watazamaji 240
walilipa sh. 30,000, 585 (sh. 20,000) na 1,423 (sh. 10,000), 614 (sh. 7,000) na
7,692 (sh. 5,000).

Baada ya kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 11,576,135.59 na gharama
za awali za mchezo ambazo ni sh. 21,843,600.00 mgawo ulikuwa kama ifuatavyo;
asilimia 10 kwa uwanja sh. 4,246,826.44, asilimia 10 kwa gharama za mchezo sh.
4,246,826.44, asilimia 5 kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh.
2,123,413.22 na asilimia 75 kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh.
31,851,198.31.

Nacho Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kilipata asilimia
tano kutoka kwa mgawo wa TFF ambayo ni sh. 1,592,559.92.
 

SEMINA YA WAAMUZI WA FIFA.
 
Semina kwa waamuzi wanaotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu
(FIFA) itafanyika Dar es Salaam kuanzia Mei 17 hadi 19 mwaka huu. Wakufunzi wa
semina hiyo ni Riziki Majalla, Leslie Liunda na Omari Kasinde.

Waamuzi hao ni Ramadhan Ibada, Waziri Sheha, Oden Mbaga, Judith Gamba na Israel
Mujuni. Waamuzi wasaidizi ni Hamis Chang’walu, Ally Kombo, Saada Tibabimale,
Josephat Bulali, Samuel Mpenzu, Erasmo Jesse, Mwanahija Makame, John Kanyenye na
Khamis Maswa.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU